30.8 C
New York

Marekani yashambulia tena meli ya mafuta

Published:

TEHRAN, Iran

Mvutano kati ya Marekani na Iran umechukua sura mpya baada ya jeshi la Marekani kushambulia meli ya mafuta katika Ghuba ya Uajemi, huku Washington ikitangaza kurejesha kizuizi cha meli zinazoingia na kutoka katika bandari za Iran.

Kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM), meli hiyo ya mafuta iliyotambuliwa kwa jina la Belma ilikuwa ikielekea katika Kisiwa cha Kharg, kituo kikuu cha Iran cha kusafirisha mafuta nje ya nchi, lakini ilipuuzia maonyo kadhaa yaliyotolewa na vikosi vya Marekani.

CENTCOM ilisema hatua ya kuisimamisha meli hiyo ilifanyika baada ya ndege za kijeshi kurusha makombora ya aina ya Hellfire yaliyolenga eneo la moshi wa meli hiyo, hatua iliyodaiwa kulenga kuizuia kuendelea na safari bila kuizamisha.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutangaza kurejeshwa kwa kizuizi cha meli zinazotumia bandari za Iran, akieleza kuwa uamuzi huo ni jibu la kile Washington inachodai kuwa ni mashambulizi ya mara kwa mara ya Iran dhidi ya meli za kibiashara zinazopita katika Mlango wa Hormuz, moja ya njia muhimu zaidi duniani za usafirishaji wa mafuta.

Tangazo hilo linakuja pia baada ya kipindi kifupi cha kusitishwa kwa mapigano kati ya Marekani na Iran, ambacho kilifuatia mashambulizi ya kulipizana yaliyoongeza hofu ya kuzuka kwa mzozo mpana zaidi katika Mashariki ya Kati.

Kabla ya hatua hiyo mpya, Marekani ilikuwa imeondoa kizuizi cha bandari za Iran pamoja na baadhi ya masharti yaliyokuwa yamewekwa dhidi ya sekta ya mafuta ya nchi hiyo, kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa Juni 17.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa sekta ya nishati, kipindi cha kulegezwa kwa vikwazo kiliiwezesha Iran kusafirisha takribani mapipa milioni 74 ya mafuta ghafi yenye thamani inayokadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni 6.

Mbali na shambulio dhidi ya meli ya Belma, CENTCOM ilisema pia ilizielekeza meli nyingine mbili za kibiashara kubadili njia baada ya mabaharia wake kufuata maelekezo ya vikosi vya Marekani.

Kurejeshwa kwa kizuizi cha bandari za Iran kunatarajiwa kuongeza mvutano katika Ghuba ya Uajemi na huenda kukawa na athari kwa usafirishaji wa mafuta duniani, hasa kupitia Mlango wa Hormuz ambao unapokea sehemu kubwa ya biashara ya mafuta ya kimataifa.

Iran haikuwa imetoa tamko rasmi kuhusu tukio hilo wakati taarifa hii inaandaliwa. Hata hivyo, wachambuzi wa siasa za kimataifa wanaonya kuwa hatua za pande hizo mbili zinaweza kuongeza hatari ya kuzorota kwa usalama katika eneo hilo na kuathiri soko la nishati duniani.

Related articles

Recent articles