Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Benki ya CRDB imesema kampeni ya kuhamasisha matumizi ya kidigitali katika kufanya miamala kupitia kadi ya Tembocard imekuwa na mafanikio makubwa.
Kampeni hiyo ya Tembocard ni Shwaa ilizinduliwa Februari mwaka huu na mpaka sasa washindi 30 wamepatikana akiwemo mkazi wa Magomeni jijini Dar es Salaam, Rahabu Mwambene, aliyejishindia gari jipya la Ford Ranger XLT katika droo ya mwisho iliyochezwa leo Julai Mosi, 2025.
Akizungumza wakati wa droo hiyo, Mkurugenzi wa Matawi wa Benki ya CRDB, Bonaventure Paul, amesema kupitia kampeni hiyo washindi 12 walikwenda Serengeti wakiwa na wenza wao na washindi watano watakwenda Ulaya.
“Benki ya CRDB imekuwa kiongozi nchini Tanzania kwa ubunifu na huduma za kisasa. Tunaendelea kuvumbua njia mpya za kuwagusa wateja wetu na kuwapa thamani zaidi ya kifedha,” amesema.
Naye Balozi wa CRDB na Msemaji wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amesema kampeni hiyo imevutia watu wengi wakiwemo mashabiki wa Simba na kutoa wito kwa Watanzania kujiunga na benki hiyo.
Kampeni ya Tembocard ni Shwaa ni sehemu ya mkakati wa Benki ya CRDB wa kusherehekea mafanikio na kukuza matumizi ya teknolojia ya kadi kwa njia ya kuvutia na yenye tija kwa wateja wake.


