8.9 C
New York

Bunge  laridhia marekebisho mpaka wa  Hifadhi ya Nyerere

Published:

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Bunge limeridhia ombi la Serikali la kumega sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kwa lengo la kutatua migogoro ya mipaka na kuwezesha shughuli za maendeleo kuendelea katika mazingira rafiki kwa jamii na uhifadhi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Hazara Chana, akiwasilisha azimio hilo bungeni, amesema kuwa Serikali imeamua kumega eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,617 kutoka Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na kulirejesha katika Pori la Akiba Selous.

Amesema hatua hiyo imepunguza ukubwa wa hifadhi hiyo kutoka kilomita za mraba 30,893 hadi kufikia kilomita za mraba 29,276.

Akifafanua zaidi,  Chana amesema hatua hiyo inalenga kuondoa migogoro ya muda mrefu ya mipaka baina ya hifadhi hiyo, vijiji vinavyoizunguka, Pori la Akiba Selous na Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori za Mbarang’andu, Juhiwangumwa, Iluma, Jukumu, Magingo na Nalika.

“Kwa kufanya hivyo, tunaimarisha usalama wa maeneo yaliyohifadhiwa, tunajenga mahusiano bora kati ya wananchi na hifadhi, na kuondoa migogoro iliyodumu kwa muda mrefu,” amesema.

Aidha, Waziri huyo ameeleza kuwa marekebisho hayo ya mpaka yanalenga kulinda mfumo ikolojia muhimu unaounganisha Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Pori la Akiba Selous, sambamba na kuhakikisha mtiririko endelevu wa maji katika Mto Rufiji, ambao ni chanzo kikuu cha uzalishaji umeme kupitia Mradi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP).

Chana amebainisha kuwa hatua hiyo itaongeza tija kwa Taifa kwa kuimarisha shughuli za utalii, uwindaji wa kitalii katika Pori la Akiba Selous na maeneo yanayozunguka, na hivyo kuchangia mapato ya ndani kupitia sekta ya utalii.

“Kwa sasa, tunaelekea katika uboreshaji wa uhifadhi wa maliasili kwa ujumla wake – wanyamapori, mimea, mazalia ya viumbe wa majini na pia kuongeza upatikanaji wa maji kwa matumizi ya wakulima, wafugaji na wavuvi,” ameongeza.
@@@

Waziri mkuu awapongeza watendaji wa Serikali kutekeleza kwa vitendo maono ya Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri mkuu  Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais  Samia Suluhu Hassan amekuwa nguzo ya kuimarisha mshikamano na umoja wa kitaifa na kufanikisha maendeleo katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wake, Rais ameweza kusimama imara katika kuendeleza miradi ya kimkakati na huduma za jamii, kusimamia demokrasia, kujenga uchumi na kuimarisha diplomasia.

Amesema hayo leo Juni 26, 2025, wakati alipotoa hoja ya kukamilisha shughuli za Bunge la 12, Bungeni jijini Dodoma.

“Sina shaka nyote mtakubaliana nami kuwa hulka yake na ustahimilivu wake umekuwa faraja kwetu sisi wasaidizi wake, watumishi wote wa umma na Watanzania wote kwa ujumla. Isitoshe, Mheshimiwa Rais wakati wote amekuwa nguzo ya kuimarisha mshikamano na umoja wa kitaifa,”

Amesema  Rais Samia amekuwa mwalimu wa subira, kielelezo cha ujasiri, ustahimilivu na alama ya matumaini kwa kizazi hiki. “Ni kiongozi aliyetoa mfano wa kuwa mwanamke anaweza kuongoza hata kwenye nafasi ya Kitaifa.”

Majaliwa amesema kuwa kutokana na uongozi dhabiti wa Rais Samia, taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa zimetambua mchango na maono yake katika kusimamia shughuli za kimaendeleo nchini na kuitangaza Tanzania nje ya nchi.

Ametaja tuzo za kimataifa  alizopokea   Rais kuwa  ni Global Gates Goalkeepers, Tuzo ya Babacar Ndiaye kwa mwaka 2022, Tuzo ya Uongozi wa Kimageuzi Afrika, Tuzo ya Heshima ya Pyne Africa Awards 2022 na Tuzo ya Muongoza Watalii Bora.

Tuzo nyingine alizopata kitaifa ni Tuzo Maalum ya Heshima ya kutambua mchango wake katika kulitumikia Taifa na kuwaletea wananchi maendeleo iliyotolewa na Bunge, Tuzo Maalum ya kutambua dhamira yake thabiti ya kujenga Taifa linalostahimili Mabadiliko ya Tabianchi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img