9 C
New York

Tamthilia Azam TV; Uhondo umeanzia walipoishia ITV

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
LEO hii, kama ni ‘mateka’ wa tamthilia za Tanzania zinazorushwa na Azam TV, basi tunaweza kusema unaiishi dunia yenye kumbukumbu nzuri ya miaka kadhaa iliyopita.
Ndiyo, katika miaka ya 2000, Azam TV haikuwepo na huenda hata wazo la kuanzishwa kwake halikuwa limefikishwa mezani.
Lakini, kituo cha televisheni cha ITV kilitufanya tuishi kwenye ‘dunia’ wanayoishi leo wapenzi wa Azam TV. Ni miaka takribani 20 iliyopita.
Kama ilivyo Azam TV kwa sasa, kituo cha televisheni cha ITV kilikuwa ‘kisima’ cha burudani kwa upande wapenzi wa sanaa ya maigizo, hasa tamthilia.
ITV ilizifanya tamthilia za Tanzania kuwa na thamani na mvuto wa aina yake, kiasi kwamba hakuna kati yetu (wapenzi wa maigizo) aliyetamani kuzikosa kila zilipokuwa zikirushwa.
Kama ilivyo sasa kwa Azam TV, haikuwa rahisi hata kidogo kutofautisha wikiendi na katikati ya wiki linapokuwa suala la burudani ya tamthilia kupitia ITV.
Mathalan, wakati ukisubiri Jumamosi ili kuwashuhudia Muhsein Awadhi ‘Dkt. Cheni’ na Fundi Said ‘Mzee Kipara’ kupitia Kaole Sanaa Group, Jumapili kulikuwa na Kundi la Chemchem la akina Mohamed Fungafunga ‘Jengua’.
Wakati huo huo, katikati ya wiki bado kulikuwa na burudani ya kutosha ya maigizo kupitia Kundi jingine la Nyota Ensemble lililokuwa na mastaa kama Bishanga Bashaija.
Kwa ufupi, ilikuwa ni ‘bandika bandua’ iliyosaidia kwa kiasi kikubwa kuwaondosha Watanzania katika utamaduni wa kupenda kazi za waigizaji wa nje, hasa Nigeria.
Kikubwa zaidi, hata asilimia kubwa ya waigizaji wanaoendelea kufanya vizuri leo hii Azam TV, waliibuliwa kupitia tamthilia zilizokuwa zikirushwa na ITV wakati huo.
Tujiulize; kama si ITV kuanzisha mwendo, wapenzi wa tamthilia wawagewafahamu Jacob Steven ‘JB’, Suzan Lewis ‘Natasha’ na wengineo wanaoendelea kufanya vizuri katika tamthilia zinazorushwa Azam TV?
Hata hivyo, kwa upande mwingine, licha ya Azam TV kupokea kijiti kutoka kwa ITV, nao wana nafasi yao, tena kubwa mno, katika safari ya tasnia ya maigizo hapa nchini.
Ni kweli ITV wataendelea kukumbukwa kwa kuasisi, lakini mchango mkubwa wa kuenziwa wa Azam TV ni namna walivyorudisha utamaduni wa kurusha tamfhilia za Bongo, ambazo wakati fulani zilionekana kupoteza dira.
Tunaweza kukubaliana kwamba Azam TV waliingia na kukuta soko la tamthilia likiwa limeshuka, kiasi cha kupoteza mvuto mbele ya wapenzi wa sanaa ya maigizo.
Tofauti na enzi zile za ITV na makundi ya Kaole, Nyota Ensemble na Chemchem, miaka ya hivi karibuni (kabla ya Azam TV kuingilia kati) haikuwa rahisi kuwakutanisha baba, mama na Watoto mbele ya runinga wakitazama tamthilia za hapa nchini.
Azam TV wamefanikiwa mno. Usiulize kuhusu ‘Kombolela’, tamthilia ya mfano kati ya zile kali zilizoteka hisia za wapenzi wa tamthilia za waigizaji wazawa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img