28.2 C
New York

Argentina v Hispania: Messi dhidi ya kivuli cha Yamal

Published:

MIAMI, Marekani

JUMAPILI ya wiki hii, Julai 19, 2026, nyasi za Uwanja wa MetLife nchini Marekani zitawaka moto kwa mchezo wa fainali ya msimu huu wa Kombe la Dunia. Argentina dhidi ya Hispania.

Ni fainali ya wababe tupu. Argentina ni bingwa mtetezi wa Kombe la Dunia na Copa America, wakati Hispania wanashikilia taji la EURO 2024.

Endapo wataifunga Hispania wikiendi hii, Argentina itakuwa timu ya kwanza kulitetea taji la Kombe la Dunia tangu Brazil ilipofanya hivyo mwaka 1962.

Hispania ilitinga fainali kwa kuifunga Ufaransa mabao 2-0, huku Argentina wakiitoa England kwa kichapo cha mabao 2-1.

Timu hizo zinakwenda kukutana kwa mara ya 15, huku Hispania ikishinda sita na kufungwa sita katika mechi 14 zilizopita. Mbili zilimalizika kwa sare.

Kwa upande mwingine, hii inakwenda kuwa mara ya kwanza kwa Lionel Messi wa Argentina kuvaana na kinda wa Barcelona, Lamine Yamal (19).

Ni wachezaji wenye historia kubwa iliyoanzia mwaka 2007, wakati huo Messi ndiyo anachipukia katika kikosi cha kwanza cha Barcelona, huku Yamal akiwa na miezi mitano tu tangu alipozaliwa.

Mwaka 2024, baada ya Yamal kuiongoza Hispania kutwaa taji la EURO, baba yake aliposti picha iliyowashangaza wengi. Picha ya Messi akiwa na mtoto mdogo wa kiume, ambaye ndiye Yamal.

Messi aliyekuwa akivaa jezi namba 19 wakati huo pale Barcelona, alianza kutumia namba 10 baada ya Ronaldinho kuondoka.

Akiwa na umri wa miaka 19, alishafunga mabao 11 na kutwaa mawili; La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kwa Yamal anayetumia jezi namba 10 pia, ana miaka 19 lakini tayari ameshafunga mabao 56, mataji matatu ya La Liga, moja la Copa del Rey, pamoja na EURO.

Related articles

Recent articles