28.2 C
New York

Wananchi wengi wanaisikia Dira 2050, lakini…

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

Licha ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuendelea kujadiliwa katika ngazi mbalimbali, bado wananchi wengi hawajaielewa kwa kina, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa umma.

Mchumi kutoka Tume ya Taifa ya Mipango, Alpha Temu, amesema uzoefu walioupata katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) unaonyesha watu wengi wamewahi kusikia kuhusu Dira hiyo, lakini hawafahamu maudhui yake wala wajibu wao katika utekelezaji wake.

“Ningeweza kusema kiwango cha uelewa ni wastani wa asilimia 60. Wengi wanasema wameisikia, lakini ukiwauliza maana yake au nafasi yao ndani ya Dira hiyo, hawana majibu ya kutosha,” amesema.

Kwa mujibu wake, hali hiyo imeonekana kupitia idadi kubwa ya wananchi waliotembelea banda la Tume ya Taifa ya Mipango na kuomba machapisho mbalimbali yanayoelezea Dira hiyo.

Tem amesema wananchi wanahitaji kuelewa kuwa Dira 2050 si hati ya Serikali pekee, bali ni mwongozo wa maendeleo wa taifa unaobainisha wajibu wa Serikali, sekta binafsi na wananchi katika kujenga uchumi wa kisasa.

Ameeleza kuwa tofauti na Dira ya mwaka 2025 iliyoandaliwa mwaka 2000, Dira ya 2050 imezingatia mabadiliko makubwa ya teknolojia, utandawazi, ushindani wa kimataifa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

“Sasa tunaishi katika dunia ambayo teknolojia imebadilisha kila kitu. Hivyo Dira hii imeandaliwa kwa kuzingatia mazingira ya sasa na ya baadaye ili Tanzania iweze kushindana kimataifa,” amesema.

Amesisitiza kuwa nyenzo zote muhimu za utekelezaji, ikiwemo mpango wa muda mrefu wa miaka 25, mipango ya miaka mitano na mipango ya mwaka mmoja, tayari zimeandaliwa, huku hatua inayofuata ikiwa ni utekelezaji kwa ushirikiano wa wadau wote.

Related articles

Recent articles