28.2 C
New York

Mwandishi mkongwe zaidi Kombe la Dunia 2026

Published:

MIAMI, Marekani

AKIWA na umri wa miaka 91 kwa sasa, Enrique Macaya Marquez ni miongoni mwa waandishi wa habari walioko Marekani wakisubiri kuripoti mechi ya msimu huu wa fainali ya Kombe la Dunia.

Mchezo wa kukata na shoka utakaozikutanisha Argentina na Hispania Jumapili hii, yaani Julai 19, 2026). 

Usichokijua kuhusu Marquez, huu ni msimu wa 18 mfululizo akienda katika nchi mbalimbali kuripoti michuano ya Kombe la Dunia.

Marquez, mwandishi wa habari wa kituo cha Redio cha DSPORTS cha Argentina, alianza kuhudhuria michuano hiyo mwaka 1958 na tangu hapo hajawahi kukosekana uwanjani.

Wakati wa fainali hizo zilizofanyika Sweden, alikuwa kijana wa umri wa miaka 24 tu na michuano hiyo ndiyo iliyompa jina Pele wa Brazil wakati timu hiyo ilipotwaa ubingwa. 

KUMBUKUMBU MBAYA

Lejendari huyo wa tasnia ya uandishi wa habari hafichi mapenzi makubwa aliyonayo kwa timu yake ya Taifa ya Argentina.

Hivyo basi, anasema moja ya matukio yaliyowahi kumuumiza katika fainali hizo ni kichapo cha mabao 6-1 walichowahi kukipata Argentina mbele ya Czech.

“Hatukuijua kabisa Czech. Hatukuwa na taarifa yoyote kuhusu timu yao, walitushitukiza na kutushangaza,” amesema Marquez.

ALIMCHUKULIA POA SCALONI

Marquez amemzungumzia kocha wa sasa wa Argentina, Lionel Scaloni, na nafasi ya timu yao kwenye mchezo ujao wa fainali ya msimu huu wa Kombe la Dunia.

Anakiri kuwa hakutegemea makubwa kutoka kwa Scaloni baada ya kocha huyo kuajiriwa mwaka 2018. “Sikuwa nikimfahamu,” amesema.

Kwa miaka nane aliyeiongoza Argentina, Scaloni ametwaa mataji makubwa matatu, likiwamo Kombe la Dunia mwaka 2022. 

Usihukumu mtu ambaye humjui,” amesema Marquez akiongeza kuwa Argentina itaifunga Hispania na kutwaa ubingwa mwaka huu.

MARADONA V MESSI

Katika maisha yake ya uandishi, amewashuhudia Diego Maradona na Lionel Messi, ambao kwa miaka mingi wamekuwa kwenye mijadala wa nani mkali wa Argentina. 

Je, Marquez amechagua upande upi? Kwa mujibu wake, hakuna namna ya kupima wachezaji waliocheza vizazi tofauti. 

“Muda ni tofauti, wapinzani ni tofauti, ubora wa timu ni tofauti. Kila mchezaji ana upekee wake. Naweza kumtaja ninayempenda lakini haimaanishi kuwa ni bora zaidi katika historia,” amesema.

Related articles

Recent articles