Na Esther Mnyika, Gazetini
MFUMO wa fedha ulio salama na unaoaminika ni nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi na kuvutia uwekezaji. Hata hivyo, mafanikio hayo yanaweza kuhatarishwa ikiwa taasisi za kifedha zitatumiwa kutakatisha fedha haramu au kufadhili ugaidi na silaha za maangamizi.
Ndiyo sababu Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kama msimamizi mkuu wa sekta ya fedha nchini, imeendelea kuimarisha mifumo ya kudhibiti utakasishaji wa fedha haramu (Money Laundering), ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa uenezaji wa silaha za maangamizi.
Utakasishaji wa fedha haramu ni nini?
Kulingana na BoT, Utakasishaji wa fedha haramu ni mchakato wa kufanya fedha zilizopatikana kwa njia zisizo halali zionekane kuwa ni halali. Mara nyingi fedha hizo hutokana na biashara ya dawa za kulevya, rushwa, utapeli, biashara haramu au makosa mengine ya kifedha.
Akizungumza na Gazetini, Afisa Sheria wa Idara ya Kuzuia Utakasishaji wa Fedha Haramu wa Benki Kuu ya Tanzania, Sheikh Naniya, anasema jukumu kubwa la BoT ni kuhakikisha sekta ya fedha haitumiki kuficha au kuhalalisha fedha zinazotokana na uhalifu.
“Lengo letu ni kuhakikisha taasisi zote zinazosimamiwa na Benki Kuu zina mifumo madhubuti ya kutambua, kuzuia na kutoa taarifa za miamala yenye viashiria vya utakasishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi,” anasema Naniya.
Jinsi fedha haramu zinavyoweza kuhalalishwa
Naniya alitoa mfano wa namna fedha haramu zinavyoweza kuingizwa katika mfumo rasmi wa uchumi.
“Mtu anaweza kupata Shilingi milioni 400 kupitia biashara ya dawa za kulevya. Ili kuficha chanzo cha fedha hizo, anaweza kutumia Shilingi milioni 50 kununua kiwanja, kisha kukitumia kama dhamana ya mkopo benki. Benki ikiridhika na nyaraka zilizowasilishwa, inaweza kumpa mkopo wa Shilingi milioni 300,” anaeleza.
Anasema baada ya kupata mkopo huo, mhusika anaweza kuunganisha fedha hizo na zile haramu kuanzisha biashara halali, kwa mfano hoteli. Baadaye mapato yanayotokana na biashara hiyo huonekana kuwa ya halali, ilhali sehemu ya mtaji wake ilitokana na fedha haramu.
Kwa nini mabenki huuliza maswali mengi?
Naniya anasema wananchi wengi hujiuliza kwa nini mabenki huomba taarifa nyingi wakati wa kufungua akaunti au kufanya miamala mikubwa.
Anafafanua kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utaratibu wa kimataifa unaojulikana kama Know Your Customer (KYC), unaolazimisha taasisi za fedha kumtambua mteja wake na kuelewa shughuli zake za kifedha.
“Benki hufuatilia mwenendo wa miamala ya wateja. Endapo kiasi cha fedha kinachoingia au kutoka hakilingani na kipato au shughuli alizojieleza, benki inaweza kuomba maelezo zaidi na, pale inapobidi, kutoa taarifa kwa mamlaka husika,” amesema.
Kwa mfano, ikiwa mtu alieleza kuwa kipato chake ni cha kawaida lakini ndani ya muda mfupi akaunti yake inaanza kupokea mamia ya mamilioni ya shilingi bila maelezo ya kuridhisha, benki inalazimika kufanya uchunguzi zaidi.
BoT inazisimamiaje taasisi za fedha?
Kwa mujibu wa Naniya, Benki Kuu hufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika mabenki na taasisi nyingine za fedha ili kuhakikisha zinafuata sheria, kanuni na miongozo ya kuzuia utakasishaji wa fedha haramu.
Taasisi zitakazobainika kukiuka sheria zinaweza kupewa onyo, kutozwa faini au hata kufutiwa leseni kulingana na uzito wa kosa.
Anasema hatua hizo zinalenga kulinda uadilifu wa mfumo wa fedha wa Tanzania na kuhakikisha sekta ya fedha inaendelea kuaminika ndani na nje ya nchi.
Tanzania imepiga hatua
Naniya anasema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mfumo wa kupambana na utakasishaji wa fedha haramu kutokana na ushirikiano kati ya serikali, Benki Kuu, taasisi za fedha na wadau wengine.
Kwa mujibu wake, mafanikio hayo yameongeza imani ya wawekezaji kwa sababu yanaonyesha kuwa Tanzania ina mfumo wa fedha unaozingatia viwango vya kimataifa vya uwazi na uwajibikaji.
Wananchi waonywa kutumia akaunti zao vibaya
Pamoja na mafanikio hayo, Naniya anabainisha kuwa bado kuna changamoto ya uelewa mdogo kwa baadhi ya wananchi, ambao wakati mwingine hukubali kupokea au kupitisha fedha kupitia akaunti zao bila kujua wanashiriki katika uhalifu wa kifedha.
“Usikubali mtu kutumia akaunti yako kupitisha fedha kwa ahadi ya kupata laki moja au mbili. Faida hiyo ya muda mfupi inaweza kukusababishia matatizo makubwa ya kisheria,” ameonya.
Amewashauri wananchi kuhakikisha wanamfahamu anayewatumia fedha na kuelewa chanzo chake kabla ya kushiriki katika muamala wowote.
“Kabla ya kukubali kufanya muamala, jiulize: Je, namfahamu mtu huyu? Je, chanzo cha fedha zake ni halali? Ukiwa na mashaka, ni bora kukataa kushiriki,” amesisitiza.
Elimu ndiyo kinga
Naniya anasema Benki Kuu imeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari, maonesho ya biashara kama Sabasaba na Nanenane, pamoja na vipindi vya redio na televisheni ili kuongeza uelewa kuhusu madhara ya utakasishaji wa fedha haramu.
Amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya uhalifu wa kifedha hayawezi kufanikiwa kwa juhudi za serikali pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa taasisi za fedha, sekta binafsi na wananchi.
“Tunapolinda mfumo wa fedha dhidi ya utakasishaji wa fedha haramu, tunalinda uchumi wa taifa, tunaimarisha mazingira ya uwekezaji na tunahakikisha mfumo wa fedha wa Tanzania unaendelea kuwa salama, wa kuaminika na wenye ushindani katika soko la kimataifa,” anasema.


