5.9 C
New York

Mramba: Miradi ya nishati itakuwa nguzo kuu kutimiza Dira ya Taifa 2050

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amekutana na wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango wakiongozwa na Naibu Katibu Mtendaji – Menejimenti ya Utendaji na Tathmini, Dk. Linda Ezekiel, kwa lengo la kujadili namna ambavyo Wizara na taasisi zake zimejipanga kutekeleza miradi ya kimkakati ya nishati inayochangia kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Msingi wa kikao hicho umetokana na Sekta ya Nishati kuainishwa katika Dira 2050 kuwa miongoni mwa vichocheo vitano vitakavyoongeza kasi ya kufikia malengo ya dira hiyo.

Imeelezwa kuwa nishati ya uhakika ni nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya viwanda na shughuli mbalimbali za kiuchumi, ili kuboresha viwango vya maisha kwa kutoa fursa za ajira na kuchochea maendeleo endelevu katika jamii.

Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma na kushirikisha watendaji kutoka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati, Mhandisi Mramba amesema pande hizo mbili zimejipanga kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa miradi ya nishati ili kuhakikisha inalingana na vipaumbele vya kitaifa vya maendeleo.

“Wizara ya Nishati inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya nishati, ukiwemo mradi wa kusafirisha umeme wa kV 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, ambao unatarajiwa kukamilika Juni 2026.

Huu ni miongoni mwa miradi itakayoleta chachu ya kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mikoa ya Katavi, Kigoma na maeneo mengine ambayo yamekuwa yakikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa umeme thabiti,” amesema Mhandisi Mramba.

Amesema kukamilika kwa miradi ya kimkakati ya umeme kutawezesha kutimiza moja ya malengo ya Dira 2050, ambayo inaelekeza kuwa matumizi ya umeme yanapaswa kuongezeka na kufikia wastani wa Kwh 3,000 kwa kila mtu kwa mwaka.

“Tunataka kuwa Taifa lenye nishati ya uhakika, nafuu na safi kwa Watanzania wote. Ili kufanikisha lengo hili, Serikali inawakaribisha wadau wa sekta binafsi kuwekeza katika miradi ya nishati, kwani mafanikio ya sekta hii yanategemea ushirikiano wa wadau wote,” amesisitiza Mhandisi Mramba.

Katika kikao hicho, Wizara pia iliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya gesi asilia na mafuta, nishati safi ya kupikia, umeme na nishati mbadala.

Kwa upande wake, Dk. Linda Ezekiel kutoka Tume ya Taifa ya Mipango amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Wizara ya Nishati na Tume hiyo, akisisitiza kuwa mwelekeo wa miradi iliyoainishwa katika kikao hicho unaendana na malengo ya Dira 2050.

Amesema Tume itaendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha inachangia moja kwa moja katika ukuaji wa uchumi wa Taifa, kuboresha ustawi wa wananchi na kulinda mazingira.

“Dira ya 2050 inalenga kuwa na Taifa lenye uchumi wa kisasa, shindani na jumuishi. Sekta ya nishati ni mhimili wa kufanikisha hayo yote. Tunapongeza jitihada za Wizara ya Nishati katika kuhakikisha nishati inakuwa injini ya maendeleo,” amesema Dk. Ezekiel.

Kupitia kikao hicho, Wizara ya Nishati na Tume ya Taifa ya Mipango zimekubaliana kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia miradi yote inayohusisha sekta ya nishati, ili kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya Dira ya Maendeleo 2050 kwa ufanisi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img