Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe, ametoa wito kwa Waganga Wafawidhi wa hospitali za rufaa nchini kuhakikisha wanazingatia mawasiliano ya awali kabla ya kumpa mgonjwa rufaa kwenda hospitali ya kanda, kwa lengo la kutoa msaada wa haraka na kuokoa maisha ya wagonjwa.
Akizungumza Agosti 21, 2025 wakati akifungua kikao kazi cha kikanda cha uboreshaji wa huduma za tiba kati ya Hospitali ya Kanda ya Benjamini Mkapa na Waganga Wakuu wa Mikoa pamoja na Waganga Wafawidhi wa hospitali za rufaa za mikoa, Dk. Magembe alisema utaratibu huo utasaidia kupunguza gharama za wagonjwa, muda wa matibabu na changamoto za usafiri.

“Kabla ya kumleta mgonjwa, tuwasiliane kwanza ili tuone kama huduma husika inaweza kupatikana kwa kubadilishana ujuzi au la mgonjwa aletwe moja kwa moja hospitali ya kanda ya Benjamin Mkapa. Hii itasaidia kupunguza mzigo wa kifedha kwa wagonjwa na kuokoa muda,” amesema Dk. Magembe.
Aidha, aliwataka waganga na madaktari kutoka mikoa na hospitali za rufaa kuwa mabalozi wa kuelimisha wananchi kuhusu huduma za kibingwa na ubingwa bobezi zinazotolewa katika hospitali ya Benjamin Mkapa, ambazo kwa sasa zimeboreshwa kwa kiwango cha juu.
Aliongeza kuwa, waganga wafawidhi wanapaswa kuhakikisha watumishi wao wanapata mafunzo ya huduma za dharura katika kituo cha mafunzo cha hospitali hiyo, ili kupunguza idadi ya rufaa zisizo za lazima na kuboresha huduma kwa wananchi.


