15 C
New York

Serikali yatenga Bilioni tisa kusomesha madaktari bingwa

Published:

*Kupunguza Rufaa nje ya nchi na kuvutia tiba utalii, Rais Dokta Samia awekeza bilioni tisa kusomesha madaktari bingwa

Na Clara Matimo, Gazetini-Mwanza

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendeleza mapinduzi katika sekta ya afya kwa kutenga jumla ya Shilingi Bilioni tisa kwa mwaka wa fedha 2025/26, kugharamia mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi kwa wataalam wa afya kupitia Samia Health Super-Specialization Program.

Akizungumza leo Agosti 21, 2025 katika ofisi za Wizara ya Afya Mtumba, jijini Dodoma, Waziri wa Afya Jenista Mhagama amesema mpango huo utagharamia ada, nauli, posho za utafiti pamoja na kujikimu kwa wanaosoma ndani na nje ya nchi, kwa mujibu wa viwango vya Wizara.

“Kwa mwaka huu tunalenga kusomesha angalau wataalam 300 wa afya katika fani mbalimbali zenye kipaumbele. Hatua hii itapunguza rufaa za wagonjwa nje ya nchi, kupunguza gharama kwa Serikali na wananchi, sambamba na kuvutia tiba utalii,” amesema Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagama amebainisha kuwa dirisha la maombi ya ufadhili limefunguliwa kuanzia Agosti 20 hadi Septemba 12, 2025 kupitia mfumo wa kielektroniki pekee katika tovuti ya Wizara ya Afya: https://esponsorship.moh.go.tz.

Kwa mujibu wa tangazo la Wizara, miongoni mwa vigezo vya kuomba ni mwombaji kuwa mtumishi wa Serikali, raia wa Tanzania, awe amepata udahili katika chuo kinachotambuliwa na Serikali, na awe anakwenda kusomea fani yenye kipaumbele kulingana na uhitaji wa kituo chake cha kazi. Waziri Mhagama amehimiza waombaji kufuatilia tovuti ya Wizara www.moh.go.tz ili kuhakikisha wanatimiza masharti yote yaliyowekwa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img