Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Dar es Salaam, Juni 25, 2025 – Licha ya juhudi mbalimbali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania, bado ni asilimia ndogo ya wananchi wanaotumia vyanzo vya nishati visivyo na madhara kwa afya na mazingira.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia za mwaka 2023, idadi ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia imeongezeka kwa kiwango kidogo kutoka asilimia 1.5 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 6.9 mwaka 2021. Kiwango hicho kipo mbali sana na wastani wa dunia ambao ulisimama kwenye asilimia 71 mwaka 2021.
Nishati zinazotambulika kuwa salama na safi kwa matumizi ya kupikia kutokana na kuwa na kiwango kidogo cha sumu ni pamoja na: umeme, bayogesi, gesi asilia, LPG (gesi ya kupikia), bayoethano, nishati ya jua, majiko banifu na mkaa mbadala wenye viwango vilivyothibitishwa na mamlaka za udhibiti wa viwango nchini.
Pamoja na mafanikio hayo ya awali, changamoto bado ni kubwa, hasa katika maeneo ya vijijini ambako wananchi wengi hutegemea kuni na mkaa wa kawaida kwa shughuli za kupikia – hali inayochangia uharibifu wa mazingira na magonjwa ya mfumo wa upumuaji kutokana na moshi unaotokana na matumizi ya nishati chafu.
Serikali na wadau wa sekta ya nishati wanahimizwa kuongeza kasi ya uwekezaji katika teknolojia za nishati safi, pamoja na elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutumia nishati salama kwa afya na maendeleo endelevu.


