26 C
New York

Miaka minne baada ya mapinduzi, Traore amefanikiwa?

Published:

OUAGADOUGOU, Burkina Faso

ALIINGIA madarakani mwaka 2022 akiliongoza jeshi kuipindua Serikali iliyokuwa madarakani. Anaitwa Kapt.
Ibrahim Traore, kijana mwenye umri wa miaka 38 tu.

Kwa upande mmoja, vijana wanamuona katika sura ya ushujaa. Kwanini? Ni kwa sera zake za kupingana na mataifa ya Magharibi, akisema yamekuwa yakiingia na kunyonya rasilimali za Afrika.

Kama itakumbukwa, muda mfupi baada ya kuingia madarakani, Traore aliwafukuza wanajeshi wa Ufaransa waliokuwa wakikabiliana na vikundi vya waasi nchini humo.

Na badala yake, kiongozi huyo akaunga utafiki na Urusi (Ulaya Mashariki), ambayo ameeendelea kushirikiana nayo kijeshi, kisiasa na hata kijeshi.

Kwa upande mwingine, Traore anayo maeneo anayoonekana kufeli kuyapatia ufumbuzi kwa miaka minne aliyokaa madarakani.

Mosi, wakosoaji wake wanauliza kuhusu hali ya usalama. Bado vikundi vya kigaidi vyenye ushirikiano na makundi ya Al-Qaeda na ISIL (ISIS) ni tatizo katika maeneo mengi ya nchi, licha ya uwepo wa operesheni za vikosi vya jeshi la Urusi.

Hata hivyo, kwa wachambuzi wa siasa kama Kabir Adamu, hali mbaya ya usalama ni tatizo la muda mrefu kwa Burkina Faso, hivyo si sahihi kumlaumu Traore na kutegemea awe amemaliza tatizo ndani ya miaka minne ya uongozi wake.

Pili, kuna ishu ya demokrasia. Wakosoaji wake wamekuwa wakimlaumu kwa uongozi wake kutokuheshimu wakosoaji, wakiwamo waandishi wa habari, wanaharakati wa haki za binadamu, n.k.

Januari, 2026, mamlaka za Burkina Faso zilitangaza kufuta vyama vya siasa zikidai kuwa vimekuwa chanzo cha mpasuko wakati nchi hiyo ikihitaji umoja na mshikamano katika kukabiliana na changamoto nyingi zilizopo.

Miezi mitatu baadaye, Traore alienda mbali zaidi na kuwataka wananchi wa Burkina Faso kusahau kuhusu demokrasia, kwa madai kuwa mfumo huo haijawahi kuisaidia Afrika, na badala yake uko kwa ajili ya kulinda masilahi ya nchi za Magharibi.

Kauli yake hiyo ilikuja wakati tayari Traore amekiuka ahadi aliyoitoa wakati anaingia madarakani mwaka 2022, ambapo alisema ataongoza kwa muda mfupi, kisha atapisha Uchaguzi Mkuu ili raia wachague Serikali yao. Ni miaka minne sasa hajatekeza hilo.

Lakini, wanamuunga mkono hawaioni hiyo kuwa ni shida kubwa. Miongoni mwao ni mwanadiplomasia wa Ghana, ambaye hata hivyo aliiomba Al Jazeera kuhifadhi jina lake kwa sababu za kiusalama.

“Nimefuatilia hotuba za viongozi wa (Afrika) Magharibi kwa miaka mingi. Traore ni wa kwanza baada ya miaka mingi kuonekana hafuati nyayo zao (kunyenyekea nchi za Ulaya),” alisema.

Kwa wanaomkubali, Traore anapita mule alimowahi kupita mwanamapinduzi Thomas Sankara, ambaye aliiongoza Burkina Faso kuanzia 1983 hadi alipouawa mwaka 1987.

Kama alivyo Traore, Sankara alionesha wazi chuki dhidi ya ukiritimba wa mataifa ya Magharibi dhidi ya Afrika na rasilimali zake.

Alitamani kuona Afrika ikisimama yenyewe, pasi na kuwekwa mfukoni na kupokea maelekezo katika maamuzi ya kisiasa, kiuchumi na hata kijamii.

Kwa sasa, wanaomuunga mkono Traore wanasema Burkina Faso imepiga hatua kubwa, wakitokea mfano uwekezaji katika sekta ya kilimo, hasa katika mazao ya mchele na mahindi.

Pia, uwekezaji katika miundombinu ya usafiri, pamoja na maendeleo ya sekta ya viwanda, ambapo uzalishaji wa ndani umekuwa kipaumbele, nayo yanatajwa kuwa alama ya utawala wake wa miaka minne.

Related articles

Recent articles