YOUNDE, Cameroon
HAJAONEKANA hadharani kwa miezi miwili sasa na wananchi wa Cameroon wanahoji; itachukua muda gani Rais Paul Biya kurudi nchini akitokea mjini Geneva, Uswis?
Wakati huo huo, wengi wana wasiwasi juu ya hali ya afya ya huyo mwenye umri mkubwa zaidi (miaka 93) duniani.
Wakati huu wananchi wakijiuliza hayo pasi na majibu, hivi karibuni Biya alifanya mabadiliko kwenye uongozi wa jeshi, hali iliyozidisha sintofahamu.
Miongoni mwa mabadiliko aliyofanya jeshini, aliyekuwa mlinzi wake tangu mwaka 2013, Raymond Jean Charles Beko’o Abondo, amepandishwa na kuwa brigedia jenerali.
Hii inakuwa mara ya nne kwa miaka ya hivi karibuni Biya kufanya mabadiliko katika uongozi wa chombo hicho cha dola.
Kama haijasahaulika, alifanya hivyo miaka mitatu iliyopita baada ya mapinduzi ya kijeshi kwa majirani zao, Gabon.
Pia, alifumua uongozi wa jeshi alipokuwa akiwania muhula wa nane madarakani katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2025.
Vilevile, itakumbukwa kuwa alifanya mabadiliko ya aina hiyo Juni, 2026, ambapo aliwapandisha ngazi baadhi ya vigogo.
Safari hii, amefanya hivyo akiwa Uswis, ambako amekuwa akiishi tangu Juni 7, 2026. Watu wake wa karibu walidai amekwenda kwa mapumziko ya muda mfupi, lakini wananchi wanaona kuna shida ya kiafya inayomsumbua kiongozi wao huyo.
Kwa walio wengi, hawafurahishwi na wanakosoa usiri wa Serikali juu ya kukaa kwake ughaibuni kwa muda mrefu, ikizingatiwa kuwa ni kuongozi wa nchi.
Mbaya zaidi, aliposhinda Uchaguzi wa mwaka 2025, Biya aliahidi kuunda Baraza jipya la Mawaziri lakini hakuna mabadiliko. Pia, nafasi ya Makamu wa Rais imebaki wazi hadi leo hii.
Kwa siku 60 akiwa nje, Biya amekuwa akiendesha Serikali akiwa Uswis, ikiwamo kutoa maelekezo ya kusainiwa kwa mikataba ya mikopo na taasisi za fedha za kimataifa.
Serikali imeendelea kusisitiza kuwa Biya hayuko kwenye matibabu kama inavyodhaniwa, lakini haitoi taarifa juu ya anachokifanya Uswis kwa muda wote huo.
Hivi karibuni, Waziri wa Habari, Rene Emmanuel Sadi, alisema kiongozi huyo yuko hai na atarejea Cameroon siku chache zijazo.
Msisitizo wa Serikali ni ule ule, kwamba Biya anaendelea na kazi akiwa ughaibuni, licha ya vyama vya upinzani, likiwamo cha CRM, kudai Rais hawezi kuwa nje ya nchi kwa muda wote huo, tena bila taarifa rasmi za anachokifanya huko.


