35.5 C
New York

Marekani, Iran: Dunia bado gizani bei ya mafuta

Published:

WASHINGTON DC, Marekani

MAREKANI imefanya shambulizi la usiku kwa mara ya tatu huko Iran. Katika shambulizi la mwisho, watu wawili wamefariki huko Kusini-Magharibi mwa Iran, jirani na Kuiwait na Iraq.

Kabla ya Marekani, tayari Iran nayo ilishashambulia meli zake mbili zilizokatiza katika Mlango-Bahari wa Hormuz mwanzoni mwa wiki hii.

Kwa mujibu wa Iran, meli hizo zilikatiza Hormuz bila kufuata utaratibu. Ni njia ya maji muhimu inayopitisha asilimia 20 ya mafuta na gesi kuingia kwenye soko la dunia.

Aidha, mashambulizi yanayofanywa na Iran na Marekani yameambatana na ujumbe wa Rais Donald Trump akisema wamezuia meli zote zinazoingia na kutoka katika bandari za nchi hiyo.

Sambamba na hilo, pia Rais Trump ametangaza kuwa kwa sasa Marekani ndiyo inayodhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz na itakuwa ikilipwa kwa kazi hiyo.

“Tutakuwa walinzi wa Mlango-Bahari huo na tutalipwa kwa kazi hiyo. Tutalipwa fedha nyingi,” amesema Rais Trump kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Truth Social.

Akisistiza kuwa kufanya hivyo ni kwa lengo la usalama, amesema Marekani itaweka wanajeshi katika eneo hilo kwa malipo ya asilimia 20 ya meli zitakazopita.

Hata hivyo, Rais Trump anafahamu wazi kuwa hatua hiyo ni kinyume cha makubaliano waliyoingia na Iran katika mazungumzo ya kusitisha mapigano yaliyofanyika wiki chache zilizopita.

Jeshi la Iran limejibu, likisema halitoruhusu Marekani kuingilia udhibiti wake wa miaka mingi katika Mlango-Bahari wa Hormuz.

Katika taarifa yake kupitia video, jeshi la Iran limesema: “Tehran haitoruhusu kwa namna yoyote ile Marekani kuingilia udhibiti wa Hormuz.”

Wakati huu makubaliano yakiwa yamepuuzwa na vita kuendelea, si Iran na Marekani pekee zinazoumia, bali hata nchi nyingi za Mashariki ya Kati.

Iran imekuwa pia ikishambulia nchi zenye urafiki na Marekani, ikiwamo Jordan ambayo jeshi lake limekiri kudondosha ndege nne za nchi hiyo.

“Ndege nne za kivita zilizoingia katika anga ya Jordan zikitokea katika mpaka wa Iran zimeangushwa,” imeeleza taarifa ya jeshi la Jordan.

Mbali na Jordan, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) nao unapitia wakati mgumu baada ya kutangaza kuwa Iran imeshambulia meli zake mbili katika Mlango-Bahari wa Hormuz.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka za UAE, shambulizi hilo limeua mtu mmoja na kujeruhi wengine nane.

UAE, moja ya nchi tajiri kwa rasilimali ya mafuta, nayo imeshambuliwa mara kadhaa na Iran kutokana na ushirika wake mkubwa na Marekani.

Vilevile, Iran imekiri kutekeleza mashambulizi dhidi ya mifumo ya rada na kambi za kijeshi zilizoko Bahrain, Kuwait na Oman.

Wakati huu vita vikiendelea, dunia imebaki gizani katika matumaini yake ya kushika kwa bei ya nishati muhimu ya mafuta.

Kwa sasa, vyanzo vya habari vya kimataifa vinaeleza kuwa bei ya pipa moja la mafuta ghafi imepanda na kufikia Dola 79.82.

Related articles

Recent articles