Na mwandishi wetu, Gazetini
HATIMAYE msimu huu 16 wa Shindano maarufu la vipaji la Bongo Star Search umefikia ukomo kwa mwimbaji Praise Wisdom kuibuka mshindi.
Mwanamuziki huyo raia wa Uganda amejiondokea na kitita cha Shilingi milioni 50, zawadi iliyoambatana na gari jipya.
Aidha, ushindi wake ni mwendelezo wa ubabe wa vipaji kutoka nje ya Tanzania kutamba kwenye mashindano hayo.
Ifahamike kuwa tangu mashindano hayo yalipoanza kushirikisha wageni mwaka 2025, hakuna Mtanzania aliyeweza kuibuka mshindi.
Msimu uliopita (2025), Moses Luka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ndiye aliyeondoka na taji na safari hii ni Praise kutoka Kampala, Uganda.
Mara ya mwisho kwa Mtanzania kuwa mshindi ni msimu wa 14 (2024), ambapo taji lilitua kwa mshiriki kutoka Arusha, Razaq Adam.
Kwa miaka mingi, Bongo Star Search imekuwa na mchango mkubwa na wa pekee katika kuibua vipaji vya muziki.
Katika kila msimu, waratibu wake wamekuwa wakija na bunifu mbalimbali zinazolifanya Shindano hilo kuwa na sura ya tofauti na kuongeza mvuto zaidi.
Baada ya kuongeza washiriki kutoka nje, safari hii Bongo Star Search ilikuja na nyongeza ya vipaji vingine nje ya muziki, ikiwamo sanaa ya vichekesho.


