33.3 C
New York

Hii ndiyo sababu ya ingia, toka ya wanawake kwa Diamond?

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

HIVI karibuni, mwanamuziki nyota kutoka Wasafi Classic Baby (WCB), Zuchu, alifichua kuachana na supastaa wa Bongo Fleva na bosi wa Lebo hiyo, Diamond Platnumz.

Zuchu alianika hayo kupitia Instagram, akiandika: “Mimi na aliyekuwa mwenzangu sasa tumetengana na tuko katika harakati za talaka.

“Namtakia aliyekuwa mwenzangu Naseeb Abdul (Diamond) na familia yake kila la kheri.”

Hata kabla ya Zuchu kuibuka na ujumbe huo, tayari minong’ono ilikuwa mingi huko mitandaoni, wengi wakihoji sababu ya bibiye huyo kutokuhudhuria sherehe ya ‘birthday’ ya mama yake Diamond.

Lakini je, ni kweli wameachana au ni ‘kiki’? Msingi wa swali hilo ni historia ya uhusiano wao ulioanza mwaka 2020.

Diamond na Zuchu wamekuwa kwenye uhusiano kwa miaka takribani sita, lakini hii si mara ya kwanza kuibuka kwa stori za kuachana.

Mathalan, Novemba 12, 2024, Zuchu aliwashitua wengi alipoibuka mitandaoni na kusema penzi lake na ‘Simba’ limefikia tamati.

Kupitia Insta, aliandika: “Baada ya miaka mitatu ya uchumba, mimi na Nasib tumeamua kuachana. Huu ulikuwa ni uamuzi wa pande zote mbili …”

Hata hivyo, waliwashangaza wengi walipoonekana tena siku kadhaa baadaye, kisha kuzima mijadala kwa kufunga ndoa mwaka 2025.

Je, ni mwendelezo wa maisha aliyochagua Diamond kwenye mahusiano?

Kwa miaka yote ya ustaa wake, Diamond amekuwa na utulivu mdogo linapokuja suala la mahusiano. Orodha ni ndefu ya warembo walioingia na kutoka kwenye maisha yake.

Kwa nyakati tofauti, mwanamuziki huyo ametoka na Wema Sepetu (Miss Tanzania 2006), Zari Hassan, Hamisa Mobetto, Tanasha Donna, Jokate Mwegelo, na Penny Mungilwa.

Katika uhusiano wake na Zari, alipata watoto wawili, Tiffah na Nillan, kabla ya kuachana mwaka 2018.

Pia, Diamond ‘Dangote’ alibahatika kupata watoto wawili, Dylan na Naseeb Jr, katika mahusiano yake na Mobetto na Tanasha.

Swali jingine; kwanini Diamond hatulii kwenye mahusiano? Baada ya kufunga ndoa na Zuchu, wengi walitarajia ungekuwa mwanzo wa utulivu wa Diamond.

Kinyume chake, ndoa imeota mbawa ndani ya mwaka mmoja. Sababu kadhaa zimekuwa zikitajwa, lakini mbili ndizo zinazohusishwa zaidi na mtindo huo wa maisha ya Diamond kwenye mahusiano.

Mosi, hata Zari ‘The Boss Lady’, alifichua kuwa sababu ya penzi lao kufa ni Diamond kutokuwa mwaminifu. Kwamba alikuwa akimsaliti kwa kuchepuka na warembo wengine.

Pili, familia ya Diamond, akiwamo mama mzazi (Mama Dangote), imetajwa mara kadhaa kuingilia na kuwa na nguvu kwenye mahusiano yake.

Licha ya kutokuwapo kwa taarifa za uhakika, changamoto za aina hiyo zilitajwa kumng’oa Mobeto na sasa zinaripotiwa kuvunja ndoa ya Zuchu.

Katika mazingira ya aina hiyo, sababu za kisaikolojia zinaweza kuhusika kwa kiasi fulani, ikizingatiwa kuwa Diamond alilelewa kwa kiasi kikubwa na mzazi mmoja (mama).

Kisaikolojia, mtoto wa aina hii humuamini, humshirikisha na kumpa kipaumbele zaidi mzazi wake, akimezwa na kumbukumbu ya maisha ya shida na mateso aliyopitia katika kumlea.

Mtoto wa aina hii anapokuwa mkubwa na kuingia katika mahusiano ya kimapenzi, mara nyingi husahau au kupuuza waziwazi nafasi na mchango wa mwenza wake.

Tabia ya usaliti inaweza kuwa moja ya njia za kuonesha dharau yake dhidi ya wanawake, akiwachukulia kama chombo cha starehe na wasiostahili hadhi na heshima aliyonayo mzazi wake.

Mwisho, swali ni je; nini hatima ya Zuchu? Ataondoka WCB au atabaki na kuendelea na kazi akiwa nje ya uhusiano na Diamond, ambaye ndiye bosi wa Lebo hiyo?

Related articles

Recent articles