33.3 C
New York

Steve Barker kuendeleza alipoishia?

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

NDANI ya muda wake mfupi ndani ya soka la Tanzania, Steve Barker ‘amesepa na kijiji’, akithibitisha kuwa ni kocha wa daraja la juu kwa namna alivyoibadilisha Simba.

Katika nusu msimu aliokaa kwenye benchi tangu alipoajiriwa Desemba 19, 2025, raia huyo wa Afrika Kusini amefanikiwa kwenye mambo kadhaa.

Simba haijapoteza mchezo tangu akae kwenye benchi. Katika mechi 25 za Ligi, ameshinda 18 na sare saba. Kwenye FA, ameshinda mechi zote sita.

Pia, Barker ameweza kurejesha soka la burudani, ambalo mashabiki walilikosa kwa muda mrefu, ikiwamo wakati wote wa kocha aliyepita, Dimitar Pantev.

Vilevile, ‘amewafufua’ baadhi ya wachezaji walioonekana wameshuka viwango, akiwamo Elie Mpanzu, ambaye wakati fulani mashabiki walifikia hatua ya kutaka aondoke.

Kama hiyo haitoshi, katika kipindi kifupi alichokaa kwenye benchi, Barker ameanza kuirejesha Simba katika meza ya mataji kwa kuipa mawili; Kombe la Mapinduzi na FA.

Kwa upande wa Ligi Kuu Bara, Barker aliipa ushindani mkali Yanga na huenda mambo yangekuwa tofauti endapo angeuanza msimu wa 2025-26 akiwa Simba.

Kwa upande mwingine, wakati mashabiki wakifurahia mafanikio yao chini Barker, mtihani alionao kocha huyo ni kuendeleza kile alichokifanya ndani ya miezi yake saba kwenye benchi.

Msimu ujao wa 2026-27, Barker hatokuwa tena mgeni wa Ligi, hivyo mashabiki wa Simba watatarajia kuona timu yao ikirejesha taji hilo lililotua Yanga kwa misimu mitano mfululizo.

Pia, kwa kuwa Barker atakuwa si mgeni tena, mashabiki watataka kuona timu yao ikilitetea taji la FA na kuianza safari ya kulibeba mara nne mfululizo au zaidi kama walivyofanya Yanga.

Aidha, kwa miaka ya hivi karibuni, Simba imejijengea heshima ya kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Watatamani kurudi huko baada ya ‘kupotea’ msimu uliopita.

Related articles

Recent articles