26.6 C
New York

Argentina v England: Nusu fainali ya chuki, kisasi

Published:

LONDON, Uingereza

NANI kutinga fainali ya msimu huu wa Kombe la Dunia katika mchezo huo wa Julai 15, 2026? Ni Argentina ya Lionel Messi au England ya Harry Kane?

Achana na Messi dhidi ya Kane au mshambuliaji huyo wa Argentina kuivaa England kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha yake ya soka.

Upande wa pili wa nusu fainali hiyo unahusisha historia iliyojaa chuki na kisasi kati ya mataifa hayo.

Iko hivi; mwaka 1966, timu hizo zilikutana robo fainali ya Kombe la Dunia pale Wembley na England kushinda bao 1-0.

Ni mechi inayowaumiza Waargentina hadi leo hii, wakiamini halikuwa bao halali kwani Geoff Hurst alifunga akiwa ‘offside’.

Mbali ya bao hilo, Waargentina wanaamini walionewa kwa kadi nyekundu aliyopewa nahodha wao, Antonio Rattin, tena ndani ya dakika 33 za kipindi cha kwanza.

Kadi ya njano ya kwanza ilitokana na kumchezea rafu Bobby Charlton na ya pili ilifuata kwa kosa la kujibishana na mwamuzi Rudolf Kreitlein.

Kama inavyoelezwa, mchezo huo ulisimama kwa dakika nane baada ya Rattin kugoma kutoka uwanjani.

Baada ya mechi kuishia, kocha wa England, Alf Ramsey, aliwakataza wachezaji wake kubadilishana jezi na wenzao wa Argentina.

Mwaka 1986, timu hizo zikakutana tena, safari hii ikiwa ni robo fainali nyingine ya Kombe la Dunia na Argentina kushinda mabao 2-1.

Waingereza waliumizwa na bao la kwanza, ambapo Diego Maradona wa Argentina alipiga kwa mkono badala ya kichwa mpira wa juu aliokuwa akigombea na kipa wa England, Peter Shilton.

Kwa kuwa mpira uliingia wavuni na mwamuzi kudhani Maradona alitumia kichwa, akaruhusu liwe bao.

Muda mfupi baadaye, Maradona aliwakera tena Waingereza. Akitokea karibu na katikati ya uwanja, aliwalamba chenga wachezaji wa timu hiyo, kisha kukutana na kipa Shilton na kuweka mpira kimiani.

Mwaka 1998, timu hizo zikakutana tena. Safari hii ikiwa ni mechi ya hatua ya 16 Bora ya Kombe la Dunia. Sare ya mabao 2-2, kisha Argentina kuingia robo fainali kwa ushindi wa penalti 4-3.

Tukio zito siku katika mchezo huo ni kadi nyekundu aliyolimwa David Beckham wa England baada ya kumpiga teke kiungo Diego Simeone.

Mwaka mmoja baadaye, Simeone (kocha wa sasa wa Atletico Madrid), alisema alijiangusha na mwamuzi kuingia ‘chaka’ kwani Beckham alistahili kadi ya njano na si nyekundu.

Mwaka 2002, timu hizo zilivaan tena, safari hii ikiwa ni mechi ya hatua ya makundi ya Kombe la Dunia. England ilishinda bao 1-0.

Mfungaji alikuwa ni Beckham kwa mkwaju wa penalti baada ya Michael Owen kuangushwa kwenye boksi na Mauricio Pochettino (sasa kocha wa Marekani).

Furaha ya Waingereza iliongezeka mara dufu baada ya Argentina kuishia hatua ya makundi, huku wao wakiingia 16 Bora.

Related articles

Recent articles