28.1 C
New York

Baba Levo: Muziki, upinzani, ‘uchawa’ hadi mjengoni

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

NI mwanamuziki? Ndiyo. Hiyo ndiyo sura yake ya kwanza iliyomtambulisha Baba Levo mbele ya walio wengi.

Achana na maisha binafsi, ambayo ndugu, jamaa na marafiki zake wanaweza kuwa na simulizi yake nyingine.

Kwa walio wengi, Clayton Revocatus Chipando aliwahi kuingia na kuishi kwenye orodha ya wasanii wa Bongo Fleva kwa upande wa muziki wa Hip hop.

Historia haioneshi kuwa aliwahi kufika katika kilele cha mafanikio ya Bongo Fleva na huenda hata yeye anaweza kukiri kwamba hakutimiza ndoto zake kwenye muziki.

Hata hivyo, historia haiwezi kumsahau katika orodha ya wasanii ambao kwa nyakati tofauti ngoma zao ‘zilisumbua’ sokoni, ikiwamo ‘Vuvuzela’.

Sura yake ya pili ni mwanasiasa wa upinzani. Akiwa ACT-Wazalendo, ndipo Baba Levo alipojenga msingi wa safari yake ya siasa.

Akianzia chini, hatimaye Chama chake kilimpitisha kugombea udiwani wa moja ya kata za Kigoma Mjini, nafasi ambayo alikuja kushinda.

Akiwa diwani kupitia upinzani, itabaki kwenye historia kuwa Baba Levo aliweka alama ya kuishi maisha ya gerezani kwa kosa la kumshambulia mtumishi wa jeshi la polisi.

Alipotoka kwenye kuta za gereza, aliendelea kwa muda mfupi kwenye siasa za upinzani, kisha kuhamisha upepo kabisa na kuja na sura yake ya tatu.

Safari hii, ni ustaa wa mitandao ya kijamii, akiwavutia wengi kwa staili yake ya aidha kusifia kupita kiasi (uchawa) au kukosoa mastaa.

Taratibu, Baba Levo akaanza kuwa na dunia yake mitandaoni. Akakusanya ‘kijiji’ chake. Akajipata na kuanza kuwa mkubwa.

Akaanza kuwa karibu na mastaa, ambao labda wengine hakuweza kuwasogelea hata alipokuwa mwanamuziki mwenzao kwenye kiwanda cha Bongo Fleva.

Sura yake hii ‘ikamfungulia dunia’ zaidi, tofauti na alivyokuwa kwenye muziki na hata siasa za upinzani kupitia ACT-Wazalendo.

Kampuni mbalimbali zikaanza kumpa dili za kutangaza bidhaa. Baba Levo wa safari hii akawa tofauti na yule wa jana na juzi na huo ukawa msingi wa sura yake ya nne.

Sura ya siasa za Chama Tawala, CCM, akiingia Bungeni kupitia mazingira yaliyompa nafasi finyu ya kushinda kiti cha ubunge.

Mazingira ambayo yalimpasa kumshinda mwanasiasa mkongwe, Zito Zuber Kabwe, kuwania kiti cha ubunge katika Jimbo la Kigoma Mjini.

Zito tayari alishakuwa mkubwa kwenye siasa za levo ya kitaifa, achilia mbali kuliongoza Jimbo hilo, lakini Baba Levo akaangusha mbuyu na kuingia ‘mjengoni’.

Leo hii, Baba Levo ni miongoni mwa vivutio vikubwa Bungeni. Si tu kwa hoja zinazopigania masilahi ya vijana na akina mama, hasa wa Jimbo lake, bali pia kwa staili yake ya uwasilishaji yenye nakshi za vituko, mbwembwe na vibwagizo.

Funzo: Katika maisha, hakuna kinachoshindikana. Kila kinachoonekana kigumu kwa macho ya kawaida, huenda ndicho rahisi zaidi kiuhalisia.

Related articles

Recent articles