MADRID, Hispania
REAL Madrid imemnasa nyota raia wa Sweden, Felicia Schroeder, na anakuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kusajiliwa kwa dau kubwa katika historia ya soka la wanawake duniani.
Madrid imeinasa saini ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 19 baada ya kuipa klabu yake ya BK Hacken kitita cha Dola milioni 1.5.
Schroeder ni miongoni mwa nyota tishio kwa soka la wanawake duniani, ambapo ameondoka Sweden akiwa ameifungia BK Hacken jumla ya mabao 91 katika mechi 128.
Msimu uliomalizika, 2025-26, alikuwa wa moto kwa mabao 30, asisti tisa katika michezo 26.
Usajili wake umelenga kuimarisha kikosi cha Madrid, ambacho msimu uliopita (2025-26) ilimaliza ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo, ikizidiwa pointi 15 na Barcelona iliyotwaa ubingwa wa Liga F.
Staa huyo kutua Madrid kumeiacha hoi Chelsea, ambayo ilikuwa ikimfukuzia baada ya kumkoa straika hatari wa Manchester City, Khadija Shaw.
Shaw ni mshindi mara tatu mfululizo wa kiatu cha michuano hiyo Super League na ndiye aliyefunga mabao mengi katika Ligi zote kubwa za Ulaya tangu alipojiunga na Man City mwaka 2021.
Hivyo, baada ya Shaw kusaini mkataba mpya Etihad, Chelsea walimtaka Schroeder na tayari walishapeleka ofa yao ya Dola milioni 1.6 kwa klabu yake ya BK Hacken.
Ikumbukwe, Blues imewapa mkono wa kwaheri washambuliaji wake, Sam Kerr na Catarina Macario, na zipo tetesi kuwa hata straika Mayra Ramirez naye ataondoka zake.
Mbali na Blues, klabu zingine zilizokuwa zikijaribu kumsajili ‘Schroeder’ ni Barcelona, Lyon, Bayern Munich, Manchester City, Juventus, Wolfsburg na Manchester United.


