JERUSALEM, Palestina
KATIKATI ya maisha magumu wanayopitia raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza, burudani ya fainali za Kombe la Dunia imepenya na kupata nafasi yake.
Wakati wa mchezo kati ya Hispania na Saudi Arabia, wengi kati ya mashabiki waliokuwa wakifuatilia kupitia runinga, walionekana kuwa upande wa akina Lamine Yamal si kuwasapoti Waarabu wenzao.
Si tu Waarabu wenzao, bali pia ni majirani zao Ukanda wa Mashariki ya Kati, ukilinganisha na umbali mrefu uliopo kati ya Palestina na Hispania.
Nyuma ya sapoti ya Wapalestina kwa timu ya soka ya Taifa ya Hispania ni siasa. Kivipi? Endelea …
Taifa hilo la Ulaya limekuwa likiwaunga mkono katika vita vyake dhidi ya Israel, ambavyo vimegharimu maisha ya Wapalestina takribani 73,000.
Tangu vita vilipoanza Oktoba, 2023, Hispania imekuwa ikisimama na Palestina kwa kulaani mashambulizi ya Israel huko Gaza.
Wiki chache zilizopita, staa wa Barcelona, Lamine Yamal, alipeperusha bendera ya Palestina baada ya timu yake kushinda moja ya mechi za La Liga.
Mwanasheria kutoka Gaza, Mohammad Attallah, anasema amekuwa akiifuatilia ‘La Roja’ (timu ya soka ya Taifa ya Hispania) kwa miaka mingi lakini mapenzi yake yamezidi kutokana na namna nchi hiyo inavyowatetea dhidi ya udhalimu wa Israel.
“Sisi ni watu wa soka. Watu wengi hapa wamekuwa wakifuatilia La Liga (Ligi Kuu ya Hispania) na timu ya Taifa ya Hispania kwa miaka mingi.
“Lakini, baada ya Hispania kuonesha msimamo wa kututetea wakati wa Vita (dhidi ya Israel), mapenzi yamekuwa makubwa zaidi,” anasema.
Hispania ni moja ya nchi zinazoshinikiza Palestina itambuliwe kama nchi huru, jambo ambalo Israel na washirika wake, ikiwamo Marekani, wamekuwa wakizuia lisitokee.
“Tunajivunia kila anayesimama upande wetu kipindi hiki (cha vita). Ndiyo maana, watu wa hapa tunaiunga mkono Hispania (kwenye Kombe la Dunia), si tu kwa sababu ya soka, bali pia kutokana na sababu za kibinadamu,” anasisitiza Attallah.
Soka halichezeki tena katika Ukanda wa Gaza kutokana na uharibifu mkubwa wa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Israel. Wachezaji wa Ligi ya ndani wamelazimika kutafuta kazi zingine baada ya viwanja vya soka kusambaratishwa kwa mabomu.


