LONDON, Uingereza
BAADA ya Keir Starmer kujiuzulu siku chache zilizopita, majina kadhaa ndani ya Chama tawala cha Labour yameanza kuhusishwa na kiti cha Waziri Mkuu wa Uingereza.
Miongoni mwao ni Andy Burnham, ambaye amewahi mara mbili kuwania na kukosa nafasi ya kukiongoza Chama hicho. Hii ni mara yake ya tatu.
Burnham ameshatangaza nia ya kuwania kiti cha uongozi wa Chama na kuwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza, akiungwa mkono na Wes Streeting aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya chini ya Keir.
Tayari Burnham ameshathibitisha nguvu aliyonayo kisiasa baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Makerfield katika Uchaguzi mdogo, ambapo Labour ilikipiku Chama cha upinzani, Reform UK, kwa kura zaidi ya 9,000.
Meya huyo wa zamani wa Jiji la Manchester, alikiwezesha Chama cha Labour kufikisha asilimia 55 ya kura, ikilinganishwa na asilimia 45 katika Uchaguzi wa mwaka 2024.
Kwa mara ya kwanza, aliingia Bungeni mwaka 2001 na tangu hapo amekuwa miongoni mwa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa ndani na nje ya Uingereza.
Burnham aliyezaliwa mwaka 1970 jijini Liverpool, ni mpenzi wa soka na shabiki kindakindaki wa klabu ya Everton.
Wazazi wake walikuwa wafuasi wa Chama cha Labour, hivyo hata yeye alianza kuvutiwa na siasa tangu akiwa mdogo. Kwa ufupi, alijiunga na Chama akiwa na umri wa miaka 14 tu.
Baada ya kuhitimu elimu ya chuo, alijitosa katika uandishi wa habari, ambapo alifanya kazi katika majarida ya biashara ya Tank World na Passenger World Management.
Akiwa na umri chini ya miaka 30, Burnham alijisogeza katika siasa alipoajiriwa kama mtafiti wa Mbunge wa Dulwich, Tessa Jowell (sasa marehemu), ambaye baadaye aliteuliwa kuwa Waziri chini ya Mawaziri Wakuu wawili, Tony Blair na Gordon Brown.
Baadaye, Burnham alipanda ngazi haraka na kuwa Mshauri Mkuu wa Katibu wa Wizara ya Utamaduni, Chris Smith, kabla ya kukwaa ubunge mwaka 2001.
Alifanya kazi chini ya utawala wa Blair, kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Hazina, kisha Katibu wa Utamaduni na Katibu wa Wizara ya Afya wakati wa Brown.
Mwaka 2010, baada ya Brown kujiuzulu, Burnham alijitosa kuwania nafasi hiyo lakini alishika nafasi ya nne kati ya wagombea watano, mshindi akiwa ni Ed Miliband.
Miaka mitano baadaye, 2015, aligombea tena nafasi hiyo lakini alianguka, safari hii Jeremy Corbyn akiibuka kidedea.
Mwaka 2017, aliwania na kushinda kiti cha Meya wa Jiji la Manchester, ambapo alishinda kwa asilimia 60 ya kura. Alishinda tena mwaka 2021.


