MEXICO CITY, Mexico
UHONDO wa mechi za fainali za Kombe la Dunia unaendelea huko Marekani, Mexico na Canada, huku yakijitokeza matukio kadhaa yaligusa hisia za wapenzi wa soka duniani kote.
Je, ni yapi hayo? Ikumbukwe, fainali hizo zilianza Juni 11 na zitafikia ukomo wake Julai 19, 2026.
HAT-TRICK YA MESSI
Nahodha wa timu ya soka ya Taifa ya Argentina, Lionel Messi, aliingia kambani mara tatu katika mchezo wao dhidi ya Algeria. Akiwa na umri wa miaka 38, amekuwa mfungaji bora wa muda wote wa Argentina katika historia ya Kombe la Dunia.
RONALDO AWAZIBA MDOMO
Katika mechi ya kwanza dhidi ya DRC, nahodha wa timu ya soka ya Taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, alikosolewa vikali kwa kiwango chake kibovu. Alirudi katika mechi ya pili (dhidi ya Uzbekistan) na kufunga mabao mawili.
CAPE VERDE SIYO POA
Ikishiriki kwa mara ya kwanza, Cape Verde ilitabiriwa kupoteza mechi zote. Kinyume chake, ilianza na suluhu (0-0) dhidi ya wababe Hispania, kisha sare ya mabao 2-2 na Uruguay.
MBAPPE BABA LAO UFARANSA
Katika mechi yao ya kwanza, walikutana na Senegal. Straika wa timu ya soka ya Taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe, alifunga mawili katika ushindi wa mabao 3-1, hivyo kuweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Ufaransa.
BALAA LA VOZINHA
Kabla ya michuano kuanza, hakuna aliyemjua kipa huyo wa timu ya soka ya Taifa ya Cape Verde. Jina lilikua fasta baada ya kuokoa mabao mengi ya wazi mbele ya Hispania. Akajipatia wafuasi milioni 15 huko Instagram.
UJERUMANI WATANGAZA KIAMA
Mechi pekee iliyoshuhudia kipigo kikubwa msimu huu ni ile ya Ujerumani kuitandika Curacao mabao 7-1. Hata hivyo, Curacao ambao wameshatoka, walionesha uwezo wa aina yake walipokwenda mapumziko wakiwa na suluhu (0-0).
BAO LA WISA KWA URENO
Ureno wakiwa mbele kwa bao 1-0 katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya DRC, shangwe zilizimwa kwa bao la kichwa la straika wa Newcastle United, Yoane Wissa. Mchezo ukaisha kwa sare ya bao 1-1.
KANE AFIKIA REKODI
Kwa bao lake la kichwa dhidi ya Croatia, Harry Kane ameifkia rekodi ya mkongwe wa timu ya soka ya Taifa ya England, Gary Lineker. Lejendari huyo alikuwa ndiye mwenye mabao mengi (10) ya Kombe la Dunia katika historia ya England.
CANADA YAPATA USHINDI
Mshambuliaji wa timu ya soka ya Taifa ya Canada, Jonathan David, alifunga ‘hat-trick’ dhidi ya Qatar. Huo ukawa ushindi wa kwanza wa Canada katika historia ya ushiriki wao Kombe la Dunia.
HAALAND KIMYAKIMYA
Akishiriki kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia, Erling Haaland alithibitisha makali yake kwa kufunga mara mbili katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Iraq. Alifunga bao la kwanza ndani ya dakika 29 tu za mchezo.


