Na mwandishi wetu, Gazetini
LICHA ya kuonekana ungekuwa mchezo mgumu, Azam FC imekubali kichapo kizito cha mabao 3-0 kutoka kwa Yanga, ambayo sasa imejishindilia kileleni mwa msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 69.
Wakati huo huo, Simba wakiwa mkoani Morogoro, wameibuka na ushindi wa aina hiyo mbele ya wenyeji wao, Mtibwa Sugar.
Azam ilipewa nafasi kubwa ya kuisumbua Yanga, ikizingatiwa kuwa ilipata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Wanajangwani hao siku chache zilizopita katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA.
Hata hivyo, katika mchezo wa leo Juni 24, 2026 wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Yanga iliondoka na pointi zote tatu kwa mabao ya Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Aurelio Depu, Pacome Zouzoua.
Kwa upande wa Wekundu wa Msimbazi, walilizamisha jahazi la Mtibwa Sugar kwa mabao ya Rushen De Reuck, Seleman Mwalimu na Anicet Oura.
Kwa matokeo hayo, vita ya ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu wa 2025-26 inabaki pale pale; Yanga iko kileleni kwa tofauti ya pointi mbili baada ya Simba kufikisha 67.
KITUO KINACHOFUATA
Baada ya ‘kuiua’ Azam, Yanga inarejea Dar es Salaam ikitokea Zenji na kujiandaa na mchezo wa Ligi unaofuata dhidi ya TRA United utakaochezwa Juni 27, 2026.
Siku hiyo hiyo, wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa, Simba, wao pia watakuwa dimbani kumenyana na Singida Black Stars.


