LOS ANGELES, Marekani
ANAITWA Marshall Bruce Mathers III lakini mashabiki wake wanamfahamu kwa jina la Eminem, ambaye ni mmoja ya mastaa wakubwa na wa muda mrefu katika ‘gemu’ la muziki wa Hip hop duniani.
Kabla ya kufikia ukubwa wa jina na utajiri alionao, Eminem, kama ilivyo kwa wasanii wengi wa Marekani, alitokea katika maisha ya hali ya chini huko mitaani mjini Detroit.
Alizaliwa Oktoba 17, 1972, baba yake akiwa mmoja ya waliokuwa wakihusishwa na magenge ya uhalifu katika mitaa ya St. Joseph, Missouri.
Hivyo, kwa sehemu kubwa ya maisha yake ya utotoni, Eminem alilelewa na mama yake, Debbie Mathers, ambaye hata hivyo hakuwa na maisha ya kumudu milo mitatu, achilia mbali nyumba nzuri na mavazi.
Maisha yake na watoto wenzake nayo yalikuwa chagamoto kubwa. Kumbuka, alikulia katika mitaa ya watu weusi, hivyo ngozi yake nyeupe ilisababisha atengwe na wenzake waliomuona siyo mwenzao.
KIPAJI TANGU UTOTONI
Licha ya umri wake mdogo wa miaka 14, tayari Eminem alishaanza kuonesha uwezo kuimba, wakati huo akionekana kuvutiwa na kazi A wakongwe LL Cool J, Run-D.M.C. na Beastie Boys.
Kama utani, Eminem alianza kuimba mitaani, akialikwa kutumbuiza katika sherehe mbalimbali, hatua iliyoendelea kuimarisha zaidi uwezo wake wa kutunga na kuimba.
Hatua kubwa zaidi ilikuja akiwa sekondari, ambako alikutana na Kimberly Anne Scott. Uhusiano wao wa kimapenzi ulikuwa na msaada mkubwa kwa Eminem kupiga hatua kimuziki.
‘Kim’ ni mrembo ambaye baadaye Eminem alimuoa na kuachana naye baada ya wawili hao kupata mtoto mmoja wa kike, Hailie, ambaye rapa huyo amekuwa akimtaja hata kwenye ngoma zake, ikiwamo ‘Hailie’s Song’ na ‘Mockingbird’.
DR. DRE AMPA RAMANI
Ilipofika mwaka 1999, ndipo jina la Eminem lilipoanza kusikika kwa sauti ya juu kwenye soko la muziki wa Hip hop alipoachia Albamu ya ‘The Slim Shady LP’ chini ya Lebo maarufu ya Aftermath Entertainment ya Dr. Dre.
Ngoma zilizotamba wakati huo ni pamoja na ‘My Name Is’ na ‘Guilty Conscience’, na haikushangaza Eminem kubeba tuzo yake ya kwanza ya Grammy katika kipengele cha Albamu Bora ya Mwaka.
Albamu yake ya pili, ‘Marshall Mathers LP’ ya mwaka 2000, iliongeza maradufu ukubwa wa jina la Eminem, ambapo si tu ilivunja rekodi ya mauzo (nakala zaidi ya milioni 1.76 ndani ya wiki moja), bali pia ilishika namba moja kwenye chati za Billboard 200.
Nyimbo kama ‘The Real Slim Shady’ na ‘Stan’ ziliendelea kumchora Eminem kama rapa bora linapokuja suala la masimulizi, kasi ya kuimba, na uwezo wa kucheza na maneno.
KUNUSURIKA KIFO, KUZALIWA UPYA
Katikati ya miaka ya 2000, wakati huo akiwa kwenye kilele cha mafanikio ya muziki baada ya kuachia albamu mbili – ‘The Eminem Show’ (2002) na ‘Encore’ (2004), staa huyo alipitia nyakati ngumu za matumizi ya kiwango cha juu cha dawa za kulevya.
Kutokana na matumizi hayo, alinusurika kifo, wakati huo pia akitajwa kuwa na changamoto ya afya ya akili. Baada ya tiba ya urahibu wa dawa za kulevya, alifanikiwa kuacha na kuwa balozi mzuri wa ishu za afya ya akili na dawa za kulevya kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Mwaka 2009, Eminem alirudi kwa nguvu sokoni kupitia Albamu ya ‘Relapse’, ambayo ndani yake kilikuwa na ngoma kali za ‘Not Afraid’ na ‘Love the Way You Lie’ aliomshirikisha Rihanna.
Tangu hapo, rapa huyo hakurudi tena nyuma, akiachia albamu kali, zikiwamo ‘Recovery’ (2010), ‘The Marshall Mathers LP 2’ (2013), ‘Revival’ (2017), na ‘Music to Be Murdered By’ (2020).


