Na mwandishi wetu, Gazetini
KATIKA utafiti wake, Kampuni ya Microsoft imebaini kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ndiyo nchi inayoongoza kwa matumizi ya ‘akili-unde’ duniani.
Kwa mwaka 2026, asilimia 70 ya watu wake wenye umri wa kufanya kazi wanatumia teknolojia hiyo, ikilinganishwa na asilimia 59.4 za mwaka 2025.
Utafiti wa Microsoft ulitazama matumizi ya walau dakika 90 kwa mtu mmoja ndani ya mwezi mmoja, ambapo Singapore imeshika nafasi ya pili kwa matumizi ya asilimia 63.4, ikilinganishwa na asilimia 58.6 za mwaka 2025.
Kwa upande mwingine, ripoti ya utafiti imeeleza kuwa matumizi ya AI yameongezea duniani. Kwamba asilimia 17.8 ya watu wenye umri wa kufanya kazi wanatumia zana za teknolojia hiyo.
Wakati Marekani ikiwa nje ya ‘Top 20’, Norway iko nafasi ya tatu ikiwa na matumizi ya asilimia 48.6 kutoka asilimia 45.3 za takwimu zilizopita (2025).
Mataifa mengine na matumizi yake kwa asilimia ni Ireland (48.4%), Ufaransa (47.8%), Hispania (44.2%), New Zealand (43.0%), Uingereza (42.2), Uholanzi (42.1%), Qatar (41.8%), Australia (39.5%), Ubelgiji (39.0%), Israel (38.1%), Uswis (37.8%), na Canada (37.3%).
Marekani, licha ya kuwa kinara wa uwekezaji na miundombinu ya AI duniani, utumiaji wake wa teknolojia hiyo ni asilimia 31.3 pekee.
Hata hivyo, bado hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya matumizi ya AI kwa raia na maendeleo ya kiuchumi ya nchi husika. Mathalan, China ina asilimia 16 pekee ya matumizi ya AI kwa watu wake, hata ikizidiwa na Thailand (36.2%) na Mongolia (32.2%).


