25.2 C
New York

Usiyoyajua kuhusu ugonjwa wa Ebola unaoitesa DRC

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

SHIRIKA la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) limetangaza hali ya dharura inayohitaji uangalizi wa kimataifa baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.

Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa tayari ugonjwa huo umeshasababisha vifo vya watu 88 na visa 336 vimeripotiwa katika mataifa mawili hayo.

Taarifa za mlipuko wa ugonjwa wa Ebola zilianzia katika Jimbo la Ituri mjini Mongwalu, Kaskazini-Mashariki mwa DRC, jirani na mipaka ya nchi za Uganda na Sudan.

Watu walioathirika na Ebola katika eneo hilo la migodi walianza kuhama na kwenda kutafuta tiba, hali iliyosababisha kuenea kwa maambukizi.

Ituri, si tu ni eneo lenye usalama mdogo kutokana na mapigano ya waasi na wanajeshi wa Serikali ya DRC, bali pia lina changamoto sugu ya uhaba wa huduma za afya.

Hivyo, kutokana na kuhama huko, maambukizi ya Ebola yalifika nchi jirani ya Uganda, ambako visa viwili vimeripotiwa kwa raia walioingia nchini humo wakitokea DRC. Mmoja alifariki mjini Kampala.

Ebola ni moja ya magonjwa hatari yanayosababishwa na virusi. Uligundulika mwaka 1976 jirani na Mto wa Ebola (sasa DRC). Virusi vya ugonjwa huo vinatokana na wanyamapori, hasa popo, na kuingia kwa binadamu.

Ugonjwa huo huambukizwa kupitia jasho, mate, damu, mbegu za kiume na matapishi. Pia, virusi vya Ebola huweza kukaa kwenye nguo au kitu chochote, kabla ya kuingia kwa mtu.

Dalili za Ebola ni pamoja na homa, kutapika, kuharisha, uchovu, maumivu ya misuli, na kuvuja damu zinazoonekana au ndani ya miwili.

Hii ni takribani mara ya 17 kwa DRC kukumbwa na janga hilo la mlipuko wa ugonjwa wa Ebola tangu virusi vyake vilipogunduliwa mwaka 1976.

Tishio kubwa zaidi la Ebola nchini humo ni lile la kati ya mwaka 2018 na 2020, ambapo watu takribani 2,300 waliripotiwa kupoteza maisha. Mwaka 2025, mlipuko mwingine uliua watu 34.

Kwa ujumla, ugonjwa wa Ebola umesababisha vifo vya watu takribani 15,000 barani Afrika tangu ulipogunduliwa mwaka 1976.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img