Na Hassan Mwasha, Gazetini
KOCHA mwenye ‘CV’ kubwa katika soka la Afrika, Florent Ibenge, ametimiza dakika dakika 20,70 tangu alipoanza kuisimamia Azam katika mechi za Ligi Kuu Bara.
Kwa hesabu rahisi, amefikisha mechi 23, kila moja ikiwa na dakika 90, tangu alipoanza kazi Septemba 24, 2025, katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City.
Katika mechi hizo, Azam imeshinda 12, sare 10 na kufungwa moja, ikifunga mabao 33 na kuruhusu tisa, hivyo inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi 46, nyuma ya Simba (52) na Yanga (54).
Ukiwa ni msimu wake wa kwanza kwenye Ligi, Ibenge ameonesha anavyomudu presha na ubabe wa vigogo wa soka la Tanzania, Simba na Yanga.
Katika mechi mbili alizokutana na Simba, ameshinda moja (2-0, Desemba 7, 2025) na kupata suluhu (0-0, Aprili 5, 2026).
Kwa upande mwingine, amekutana na Yanga mara moja (Machi 15, 2026) msimu huu na dakika 90 za mchezo huo zilimalizika kwa suluhu.
Hata hivyo, moja ya machungu aliyopata Ibenge ndani ya Ligi Kuu Bara ni kile kilichotokea Mei 8, 2026, ambapo Azam yake ilifungwa mabao 4-1 na TRA United.


