22 C
New York

Museveni amekana kivuli chake akiwa amesahau au makusudi?

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

RAIS Yoweri Museveni ameapishwa kuanza awamu yake ya saba baada ya ushindi katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Januari, 2026, akiandika historia ya kuwa mmoja ya viongozi waliodumu Ikuku kwa miaka mingi.

Hafla ya kuapishwa kwake mjini Kampala iliambatana na ulinzi mkali, huku Rais huyo mwenye umri wa miaka 81 akiahidi makubwa katika awamu yake ya saba.

“Tunapaswa kulinda mafanikio tuliyopata, kurekebisha pale panapohitaji maboresho na kusonga mbele kama Taifa moja,” alisema katika hotuba yake.

Ushindi wake wa asilimia 70 ya kura katika Uchaguzi uliogubikwa na vurugu za hapa na pale, hasa baada ya matokeo kutangaza, utamuweka madarakani hadi mwaka 2031.

Itakumbukwa, mpinzani wake, Bobi Wine, aligomea matokeo kwa kile alichokiita ‘wizi wa kura’, madai ambayo hata hivyo yalipuuzwa na Tume ya Uchaguzi.

Haikuishia hapo. Wine (44), ambaye pia ni nguli wa muziki, alilazimika kukimbia nchi baada ya Uchaguzi akisema anahofia ‘kupotezwa’ na utawala wa Rais Museveni.

Wakati huo huo, ripoti za taasisi za haki za binadamu ziliripoti juu ya kuuawa kwa watu 16 walipoteza maisha wakati wa Uchaguzi.

Moja ya taasisi hizo, Amnesty International, ililaani pia mashitaka dhidi ya mwanasiasa mkongwe wa upinzani, Kizza Besigye, ambaye alikamatwa nchini Kenya na kurudishwa Uganda.

Museveni, kwa upande wake, ameshinda chaguzi saba tangu alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 1986.

Ni miongoni mwa marais walioziongoza nchi zao kwa miaka zaidi ya 40, akiwamo Denis daily themed Sassou Nguesso (Congo-Brazzaville), Teodoro Obiang (Guinea ya Ikweta) na Paul Biya (Cameroon).

Rais Museveni aliyezaliwa mwaka 1944 akitokea katika familia masikini iliyojihusisha na ufugaji, ni kama amesahau au kwa makusudi ameamua kukana kivuli chake.

Mwanzoni mwa safari yake ya siasa na hata akiwa Tanzania alikosomea Uchumi na Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alijitanabaisha kuwa ni mwanasiasa aliyekerwa na utawala wa kidikteta wa Idi Amin aliyekuwa akiiongoza Uganda.

Aliporejea Uganda, aliunda kundi la waasi lililoingia vita na kumng’oa madarakani Amin. “Alikuwa sehemu ya mifumo ya wakoloni,” alisema Museveni.

Baada ya anguko la Amin, Milton Obote alirejea madarakani kupitia Uchaguzi Mkuu, ingawa Museveni alipinga matokeo akidai ‘aliiba kura’ kupata ushindi.

Hivyo, Museveni aliunda Kundi la National Resistance Movement (NRM) na kuingia msituni kwa lengo la kuanzisha vita ya kuung’oa utawala wa Obote.

Mwaka 1986, Museveni akaingia Ikuku.

Hapo ndipo aliposema: “Tatizo la Afrika kwa ujumla, siyo watu, bali viongozi wanaong’ang’ania madaraka.”

Ikiwa ni miaka zaidi ya 40 tangu alipotoa kauli hiyo, leo hii wakosoaji wake wanamtazama Museveni kama kiongozi wa aina ile ile, anayetaka kubaki Ikuku milele, tena kwa gharama ya yoyote, ikiwamo umwagaji wa damu wa raia kila kinapofika kipindi cha Uchaguzi.

Mwaka 2017, katika kutimiza matarajio yake ya kubaki Ikulu, Museven alishinikiza na kufanikisha mabadiliko ya Katiba, akiondoa kipengele cha umri.

Kama hiyo haitoshi, Museven anatajwa ‘kuziweka mfukoni’ taasisi kama Mahakama, ambazo kimsingi zinapaswa kujitegemea.

Wachambuzi wa siasa nchini Uganda wanaona hii inaweza kuwa awamu ya mwisho kwa Rais Museveni kuiongoza Uganda.

Hata hivyo, bado wengi wanaamini kuna uwezekano mkubwa wa mtoto wake wa kiume, Muhoozi Kainerugaba, ambaye kwa sasa ndiye mkuu wa majeshi, kurithi kiti chake.

Jenerali huyo amekuwa akikosolewa vikali kwa namna ambavyo amekuwa akiwakandamiza wanasiasa wa upinzani, akiwamo Wine.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), aliwahi kutishia kutoa nyeti za Wine anayekiongoza Chama cha National Unity Platform. Alifuta posti hiyo baadaye.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img