22 C
New York

Hasara ATCL yaongezeka maradufu, yafikia Sh Bilioni 191.19

Published:

Na mwadishi wetu, Gazetini

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini kuwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limeendelea kupata hasara kubwa, ambapo katika mwaka wa fedha 2024/2025 shirika hilo limepata hasara ya sh bilioni 191.19.

Akiwasilisha ripoti hiyo leo Machi 30, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, CAG Charles Kichere amesema kiwango hicho cha hasara ni ongezeko la asilimia 108 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Kwa mujibu wa Kichere, hali hiyo imeifanya jumla ya hasara ya ATCL tangu kuanzishwa kwake kufikia shilingi bilioni 748, jambo linaloibua maswali kuhusu uendelevu wa kifedha wa shirika hilo.

“Hasara imeongezeka kutokana na changamoto mbalimbali za kiutendaji, ikiwemo gharama za uendeshaji kuzidi ukuaji wa mapato pamoja na ufanisi mdogo wa safari za ndege,” amesema Kichere.

Amefafanua kuwa licha ya serikali kuendelea kutoa ruzuku kwa ajili ya kulipia mishahara na gharama za uendeshaji, ATCL bado inakabiliwa na mzigo mkubwa wa matumizi, ambapo gharama za uendeshaji zimeongezeka kwa sh bilioni 134 na kufikia jumla ya sh bilioni 675.

Ripoti hiyo pia imebainisha kuwa ufanisi wa safari za ndege uko chini ya kiwango kinachotarajiwa, huku wastani wa ujazo wa abiria (load factor) ukiwa ni asilimia 55 pekee katika jumla ya njia 87 zinazohudumiwa na shirika hilo.

“Katika njia 87 za safari, wastani wa ujazo wa abiria ulikuwa asilimia 55, hali inayoonyesha kuwa ndege nyingi hazijajazwa ipasavyo na hivyo kupunguza mapato,” ameeleza.

Kwa upande wa usafirishaji wa mizigo, Kichere amesema matumizi ya ndege ya mizigo aina ya Boeing 767-300F hayakuwa bora, kwani asilimia 94 ya safari zake zilikuwa za masafa mafupi na ya kati badala ya safari ndefu zenye tija kubwa ya mapato.

Ameongeza kuwa hali imezidi kuwa mbaya baada ya ndege hiyo kusimamishwa kufanya kazi, huku ikiendelea kugharimu shirika takriban sh bilioni 3.54 kwa ajili ya ukodishaji na bima bila kuingiza mapato yoyote.

Wakati huo huo, ripoti imebaini udhaifu katika mifumo ya udhibiti wa ndani, ikiwemo malipo ya sh bilioni 20.61 yaliyofanywa kwa mawakala wa tiketi bila kuwepo kwa uthibitisho wa kuwafikia abiria husika.

Matokeo hayo yanaibua haja ya hatua za haraka za kiutawala na kimkakati ili kuboresha ufanisi na kupunguza hasara ndani ya shirika hilo la taifa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img