CALIFORNIA, Marekani
BAADA ya timu ya soka ya Taifa ya Ureno kulazimishwa sare ya bao 1-1 na DRC, lawama zote zilielekezwa kwa nahodha wa kikosi, Cristiano Ronaldo.
Kelele dhidi yake zilitokana na kiwango duni alichokionesha katika mchezo huo wa hatua ya makundi msimu huu wa Kombe la Dunia.
Katika dakika 65 alizocheza staa huyo mwenye umri wa miaka 41, alipiga mashuti manne, alikosa mabao matatu ya wazi na alipoteza mipira mara nne.
Wengi, akiwamo wakongwe wa Manchester United na Arsenal, Paul Scholes na Thierry Henry, wakisema Ronaldo aliigharimu kwa kiasi kikubwa Ureno katika mechi hiyo.
Hata hivyo, kama ilivyo kawaida, nyuma yake alisimama mrembo aitwaye Katia Aveiro, ambaye aliibuka na kumtetea.
Aveiro (46), ambaye ni dada yake wa kwanza, aliibuka huko mitandaoni na kusema hakuona mchezaji yeyote wa Ureno aliyecheza vizuri katika mchezo huo.
“Kwa kweli, nikiwa kama shabiki wa nchi yangu, nimesikitishwa. Hatukucheza vizuri, hakuna aliyecheza vizuri,” alisema Aveiro.
Kwa mashabiki wa soka, hii haikuwa mara ya kwanza kumuona Aveiro ‘akivaa mabomu’ kumtetea mwanasoka huyo anayekipiga Al Nassr ya Saudi Arabia.
Baada ya Lionel Messi kutwaa tuzo ya nane ya Ballon d’Or, bibiye huyo aliingia mitandaoni na kusema Ronaldo ndiye aliyestahili kuichukua.

Katika kumchokoza Messi, Aveiro ambaye ni mama wa watoto watatu, aliposti picha ya Ronaldo akiwa na mataji mengi aliyowahi kutwaa na kusindika na ujumbe unaosomeka: “Ameshinda, siyo kupewa.”
Kama hiyo haitoshi, alisema fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2022 ndizo mbovu zaidi kuwahi kutokea. Ni wakati ambao Argentina ya Messi ilitwaa ubingwa.
Aveiro ndiye mtoto mkubwa katika familia yao, akifuatiwa na bibiye Elma na Hugo ambaye ni wa kiume. Ronaldo ndiye mdogo zaidi.
Katika ndoa yake na Jose Pereira, bibiye huyo alibahatika kupata watoto wawili wa kiume – Rodrigo (24)na Dinis (14).
Kwa sasa, anatoka na mfanyabiashara maarufu wa Brazil, Alexandre Bertolucci, ambapo wanaishi nchini humo na mtoto wao mmoja tangu walipoingia kwenye mahusiano mwaka 2019.


