Na Faraja Mulungu, Gazetini
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imemhukumu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kifungo cha miaka minne jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la uchochezi katika kesi iliyokuwa ikimkabili ya uhaini.
Hukumu hiyo imetolewa leo, Ijumaa, Novemba 6, 2026, na kuhitimisha shauri lililodumu kwa takribani miezi 19 siku zisizopungua 500,tangu Lissu alipokamatwa Aprili 9, 2025.
Katika uamuzi wake, mahakama haikumtia hatiani Lissu kwa kosa la uhaini, lakini ilimkuta na hatia ya kosa dogo la uchochezi.
Lissu alikuwa akikabiliwa na shtaka la uhaini katika kesi namba 000019605 ya mwaka 2025, akishtakiwa kwa kukiuka Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, mjini Mbinga, mkoani Ruvuma, muda mfupi baada ya kuhutubia mkutano wa Chadema uliokuwa sehemu ya kampeni ya chama hicho ya “No Reforms, No Election”.
Siku iliyofuata, Aprili 10, 2025, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, na kusomewa shtaka la uhaini.
Mashtaka hayo yalihusiana na matamshi aliyodaiwa kutoa Aprili 3, 2025, katika mkutano na wagombea wa Chadema uliofanyika katika ofisi za chama hicho, Mikocheni, Dar es Salaam.
Upande wa mashtaka ulimtuhumu Lissu kwa kutoa matamshi na kuchapisha taarifa zilizolenga kuchochea umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, kwa nia ya kuitishia Serikali. Lissu alikana mashtaka hayo.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa rasmi katika Mahakama Kuu Septemba 8, 2025, mbele ya jopo la majaji watatu lililoongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Katika kipindi cha usikilizwaji, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 17 kati ya 30 waliokuwa wameorodheshwa, huku Lissu akiwasilisha mashahidi watano kwa upande wa utetezi.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa mahakamani ni matamshi aliyodaiwa kutoa Lissu, ushahidi wa video ya mkutano huo ambayo haikuwasilishwa mahakamani, namna video hiyo ilivyosambazwa pamoja na tafsiri ya kisheria ya kosa la uhaini.
Agosti 21, 2026, mahakama iliamua kuwa Lissu alikuwa na kesi ya kujibu na kumtaka ajitetee. Uamuzi huo haukumaanisha kuwa tayari amepatikana na hatia, bali ulifungua hatua ya utetezi katika shauri hilo.
Baada ya utetezi kukamilika, pande zote ziliwasilisha hoja zao za mwisho. Utetezi uliwasilisha hoja zake kati ya Septemba 23 na 28, 2026, kabla ya upande wa mashtaka kuhitimisha hoja zake Septemba 29, mwaka huo.
Katika hukumu ya leo, mahakama imeeleza kuwa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka haukuthibitisha bila kuacha shaka kuwa Lissu alikuwa na nia ya kuitishia Serikali, ambayo ni sehemu muhimu ya kuthibitisha kosa la uhaini.
Mahakama pia ilitathmini matamshi yaliyodaiwa kutolewa na Lissu kuhusu kuzuia uchaguzi na kuchochea wananchi kutotii Serikali, ikieleza kuwa masuala hayo yanapaswa kutofautishwa katika uchambuzi wa kisheria.
Hata hivyo, mahakama ilimkuta na hatia ya kosa dogo la uchochezi na kumhukumu kifungo cha miaka minne jela. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, kosa hilo linaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha juu cha miaka mitano jela.


