NAIROBI, Kenya
MHUBIRI wa Kenya, Paul Nthenge Mackenzie, amehukumiwa kifungo cha miaka 200 gerezani kutokana na nafasi yake katika mauaji ya watu 191, wakiwemo watoto 190, yaliyotokea katika Msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi nchini Kenya.
Hukumu hiyo imetolewa Ijumaa, Novemba 6, 2026, na Mahakama Kuu ya Mombasa, ambapo Jaji Diana Kavedza alimkuta Mackenzie na hatia ya makosa 191 ya mauaji yaliyohusishwa na vifo vya waumini hao kati ya Januari 2021 na Septemba 2023.
Mackenzie, ambaye ni mwanzilishi wa kanisa la Good News International Church, alihusishwa na kuwashawishi wafuasi wake kuacha makazi yao na kwenda kuishi katika Msitu wa Shakahola, akiwahimiza kufunga chakula kwa madai kuwa kufanya hivyo kungewasaidia kumkaribia Mungu na kujiandaa kwenda mbinguni.
Katika uamuzi wake, mahakama ilieleza kuwa Mackenzie alikuwa na jukumu kubwa katika vifo hivyo kwa kuwa ndiye aliyewaelekeza wafuasi wake kufunga hadi kufa, huku baadhi ya waliopinga mafundisho yake wakikabiliwa na vipigo na vitendo vya ukatili.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Mackenzie amehukumiwa miaka 100 jela kwa makosa ya mauaji yaliyotokana na kuwafanya waumini kufunga hadi kufa, pamoja na miaka mingine 100 kwa makosa ya mauaji ya moja kwa moja dhidi ya watoto, hivyo kufanya jumla ya adhabu yake kufikia miaka 200 gerezani.
Jaji Kavedza alisema adhabu hiyo imezingatia uzito wa makosa, mazingira ya vifo vya waathiriwa na madhara makubwa yaliyosababishwa kwa manusura, familia zilizopoteza ndugu zao na jamii kwa ujumla.
Awali, upande wa mashtaka ulikuwa umeiomba mahakama imhukumu Mackenzie adhabu ya kifo kutokana na ukubwa wa uhalifu huo. Hata hivyo, ombi hilo lilikataliwa na Jaji Kavedza, aliyeeleza kuwa adhabu ya kifo ingeondoa uwezekano wa mabadiliko ya tabia na marekebisho kwa mfungwa.
Ushahidi uliowasilishwa mahakamani ulionyesha kuwa baadhi ya wafuasi wa Mackenzie walimwamini kama msemaji wa Yesu, huku watoto wakifanyiwa ukatili wa kimwili ili kuwalazimisha kutii maagizo ya kufunga.
Uchunguzi wa miili ya waathiriwa ulionesha kuwa wengi walifariki kutokana na njaa, huku wengine wakipoteza maisha kwa kukosa hewa, kunyongwa au kupata majeraha ya kichwani. Katika baadhi ya miili, wataalamu walishindwa kubaini chanzo cha kifo kutokana na hali ya kuharibika kwa miili hiyo.
Mauaji ya Shakahola ni miongoni mwa matukio mabaya zaidi yanayohusishwa na misimamo mikali ya kidini nchini Kenya, na kesi hiyo imeibua mjadala kuhusu udhibiti wa taasisi za kidini na wajibu wa mamlaka katika kuzuia mafundisho yanayohatarisha maisha ya waumini.


