Na mwandishi wetu, Gazetini
JAJI Dunstan Ndunguru ameanza kutoa maelezo ya msingi wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, kabla ya kutangaza hukumu.
Akisoma maelezo ya shitaka, Jaji Ndunguru amesema Lissu anatuhumiwa kuwa Aprili 3, 2025, katika Wilaya ya Kinondoni, akiwa na utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitengeneza nia ya kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa lengo la kuitishia Serikali.
Katika maelezo ya shitaka hilo, mahakama imetaja kauli inayodaiwa kutolewa na Lissu kuwa: “Ni kweli, sababu tutaahamasisha uasi … tunaenda kukinukisha sana sana tutauvuruga huu uchaguzi.”
Jaji Ndunguru ameeleza kuwa Lissu aliposomewa shitaka hilo alikana, na hivyo shauri likaingia katika hatua ya kusikilizwa.
Amesema jukumu la kuthibitisha shitaka lilikuwa kwa upande wa mashitaka, uliowakilishwa na mawakili wa Serikali, akiwemo Nasoro Katuga na wenzake.
Upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi 17, wakiwemo mashahidi wa kificho kwa mujibu wa sheria, huku Lissu akijitetea mwenyewe na kuwasilisha mashahidi pamoja na vielelezo vyenye maelezo ya mashahidi wa mashitaka namba moja hadi 16.
Jaji Ndunguru amesema baada ya ushahidi wa pande zote mbili kukamilika, upande wa mashitaka na utetezi waliwasilisha hoja zao za mwisho (final submissions) kwa ajili ya kuhitimisha usikilizwaji wa kesi hiyo.


