Na Mwandishi Wetu, Accra, Ghana
WAZIRI wa Madini, Anthony Peter Mavunde, amezitaka nchi za Afrika kutumia rasilimali na mapato ya ndani kufadhili maendeleo ya sekta ya madini, kuanzia utafiti wa kijiolojia hadi uchakataji na usafishaji, badala ya kutegemea zaidi mitaji kutoka nje ya bara hilo.
Mavunde ameyasema hayo Oktoba 20, 2026, jijini Accra, Ghana, alipokuwa akiongoza kikao cha mawaziri wa Afrika katika mkutano wa Mining in Motion 2026, kilichojadili namna ya kupata fedha za kuendeleza mnyororo mzima wa thamani wa madini.
Akizungumzia uzoefu wa Tanzania, Mavunde amesema Serikali imetenga asilimia 10 ya mapato yatokanayo na sekta ya madini kwa ajili ya utafiti wa kina wa kijiolojia, hatua inayolenga kubaini na kuongeza uelewa wa rasilimali zilizopo nchini.

Amesema takribani asilimia 16 pekee ya eneo la Tanzania limefanyiwa utafiti wa kina, hali inayoonyesha umuhimu wa kuwekeza zaidi katika utafiti ili kubaini maeneo mapya yenye uwezekano wa kuwa na madini.
“Utashi wa kisiasa uliooneshwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wa kutenga asilimia 10 ya mapato yatokanayo na sekta ya madini kwa ajili ya utafiti wa kina ni hatua muhimu katika kupunguza utegemezi wa fedha za wahisani na kuwezesha Tanzania kufadhili utafiti wa rasilimali zake kwa kutumia mapato ya ndani,” amesema Mavunde.
Amesisitiza kuwa ufadhili wa sekta hiyo haupaswi kuishia katika utafiti na uchimbaji, bali unapaswa kuhusisha pia ujenzi wa viwanda vya uchakataji na usafishaji wa madini ili kuongeza thamani kabla ya bidhaa hizo kuuzwa.
Kwa mujibu wa Mavunde, uwekezaji katika viwanda hivyo unaweza kuongeza ajira, kukuza ujuzi wa Watanzania na kuongeza mapato yatokanayo na mauzo ya madini yaliyoongezwa thamani.
Aidha, amesema Tanzania inaendelea kuimarisha ushiriki wa wazawa kupitia mfumo wa maudhui ya ndani (Local Content), unaolenga kuongeza nafasi za kampuni za Kitanzania katika kutoa bidhaa na huduma kwa migodi.
Ameeleza kuwa mafanikio ya sekta ya madini yanahitaji ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za fedha na sekta binafsi, pamoja na uwekezaji katika miundombinu na mifumo bunifu ya ufadhili.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi na Rasilimali Asili wa Ghana, Emmanuel Armah-Kofi Buah, amezitaka nchi za Afrika kushirikiana kukabiliana na changamoto za mitaji, miundombinu na nishati, huku zikiongeza thamani ya madini na kulinda maslahi ya jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.
Wito huo umeelekezwa katika kujenga uwezo wa Afrika kufadhili miradi yake ya madini, kuendeleza viwanda na kunufaika zaidi na rasilimali zake.


