20.3 C
New York

Don King: Promota mwenye heshima, skendo ya ‘kuwapiga’ mabondia

Published:

LOS ANGELES, Marekani

KAMA ni mfuatiliaji wa mchezo wa ndondi, basi jina la Donald ‘Don’ King haliwezi kuwa geni masikioni mwako. Ni promota mwenye umaarufu wa aina yake si tu Marekani, bali ulimwenguni kote.

Anafahamika kwa kufanikisha mapambano mengi makubwa katika historia ya mchezo wa ngumi, yakiwamo mawili maarufu zaidi; ‘The Rumble in the Jungle’ na ‘Thrilla in Manila’.

The Rumble in the Jungle ni pambano zito lililowakutanisha wababe Muhammad Ali na George Foreman nchini Zaire [sasa ikiitwa DRC], ikielezwa kuwa Don King alivuna mkwanja mrefu wa Dola milioni 10.

Baadaye, promota huyo aliitikisa tena dunia alipoandaa pambano jingine kubwa la Thrilla in Manila. Ni vita ya ulingoni iliyowakutanisha wakali wawili wa wakati huo, Ali na Joe Frazier, mjini Manila, Ufilipino.

Kwa nyakati tofauti, Don King aliwahi kufanya kazi pia na mabondia wengine wakali, wakiwamo Mike Tyson, Evander Holyfield na Julio Cesar Chavez.

Lakini, licha ya mafanikio, pia Don King amewahi kukwaa skendo kadhaa, ikikumbukwa kuwa hata Tyson aliwahi kumtolea uvivu akisema alikuwa akipendelea mabondia wa kizungu.

Kama hiyo haitoshi, Muhammad Ali aliwahi kumfungulia kesi ya kumlipa fedha kiduchu katika pambano lake dhidi ya bondia Larry Holmes. Don King alikiri na kisha kulipa fidia ya Dola 50,000.

Pia, lejendari wa ndondi, Larry Holmes, aliwahi kudai kuwa King alimdhulumu si chini ya Dola milioni 10 katika mapambano yote aliyomsimamia. Alisema aliambulia Dola 150,000 kati ya Dola 500,000 za pambano lake na Ken Norton.

Vilevile, Don King ana historia ya kuua mfanyakazi wake kwa kichapo kwa madai kuwa alimuibia kitita cha fedha cha Dola 600. Alikutwa na hatia na kutumikia kifungo cha miaka mitatu na miezi 11 gerezani.

Dong King bado anaishi lakini mkewe, Henrietta, alifariki Desemba 2, 2010, akiwa na umri wa miaka 87, wakati huo wakiwa wamebahatika kupata watoto wawili na wajukuu watano.

Nje ya ulingo, ni mfuasi mkubwa wa siasa na alikuwa upandewa Barack Obama wakati wa mbio za urais katika chaguzi za mwaka 2008 na 2012.

Kabla ya Obama, Dong King alionekana mara kadhaa kwenye mikutano ya kampeni akimuunga mkono George W. Bush na kwa sasa ni shabiki wa Donald Trump.

Related articles

Recent articles