19.5 C
New York

Wakulima Kagera watakiwa kuchagua miche bora ya kahawa

Published:

Na Editha William – Kagera

Wakulima wa kahawa mkoani Kagera wameshauriwa kuzingatia ubora na afya ya miche wanayoichagua kwa ajili ya kupanda ili kuepuka changamoto za uzalishaji, ikiwemo kusambaa kwa magonjwa ya kahawa mashambani.

Ushauri huo umetolewa na Afisa Kilimo wa Shirika la Strategies for International Development (SID) Tanzania, Dativa Frankilin, aliyesema wakulima wanapaswa kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu sifa za miche bora wanapofika kwenye vitalu kabla ya kufanya uchaguzi.

Akizungumza na mwandishi wetu, Dativa amesema ni muhimu wakulima kununua miche kutoka kwenye vitalu vilivyoidhinishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TAKRI) pamoja na Bodi ya Kahawa, ili kuhakikisha wanapata miche yenye afya na kupunguza hatari ya kusambaza magonjwa mashambani.

Amesema baadhi ya wakulima wanaootesha miche katika vitalu vyao binafsi wanaweza kukosa elimu na utaalamu wa kutosha kuhusu namna bora ya kuandaa na kutunza miche, hali inayoweza kusababisha miche hiyo kuwa chanzo cha kusambaa kwa magonjwa ya kahawa.

“Mkulima aliyeotesha miche kwenye kitalu chake anaweza asiwe na elimu ya kutosha katika uoteshaji wa miche hiyo, hivyo kupelekea kuwa chanzo cha usambazaji wa magonjwa ya kahawa kwa miche mingine shambani,” amesema Dativa.

Ameongeza kuwa kupanda miche dhaifu kunaweza kumsababishia mkulima hasara ya mazao pamoja na kupoteza muda na gharama alizotumia katika msimu mzima wa uzalishaji.

Kutokana na hali hiyo, amewashauri wakulima ambao hawana elimu ya kutosha kuhusu uchaguzi na upandaji wa miche kuwasiliana na maafisa ugani ili kupata maelekezo sahihi na kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza shambani.

Ametaja baadhi ya vigezo vya kuchagua miche bora kuwa ni kuangalia mwonekano na afya ya mche, pamoja na kuhakikisha umefikia umri unaofaa kwa ajili ya kupandwa, ambao ni kati ya miezi sita na tisa.

Aidha, amewakumbusha wakulima kutenganisha udongo wa juu wenye rutuba na udongo mwekundu wakati wa kuchimba mashimo ya kupandia, ili kuhakikisha mche unapata udongo wenye rutuba na kustawi vizuri shambani.

Related articles

Recent articles