LOS ANGELES, Marekani
MOJA ya stori zilizotikisa tasnia ya burudani nchini Marekani ni hii ya mke wa zamani wa rapa Eminem, Kim Scott, kukimbizwa hospitali.
Katika tukio hilo la wikiendi iliyopita, polisi waliopigiwa simu na majirani walifika nyumbani kwake Michigan na kumkuta ndani akiwa amepoteza fahamu.
Ni miezi miwili tu imepita tangu bibiye huyo mwenye umri wa miaka 51 alipoharibu Range Rover yake kwa kuligonga gari jingine kwenye eneo la maegesho.
Mtandao wa udaku wa TMZ uliripoti kuwa siku hiyo Kim alikuwa kwenye gari na mtoto wake wa kiume, Parker, aliyeambatana na marafiki zake watatu.
Polisi walimfungulia mashitaka mawili; kuendesha gari akiwa amelewa na kukimbia baada ya ajali hiyo.
Siku chache baadaye, Kim alikamatwa kwa kosa la kutokuhudhuria mahakamani wakati wa usikilizwaji wa shitaka hilo. Alitozwa faini ya Dola 10,000.
Kim na Eminem ni marafiki wa utotoni, tangu rapa huyo akiwa anasoma. Mama yake Eminem, Debbie Nelson, aliwahi kusimulia kuwa Kim alitoroka kwao na wakawa wanaishi naye.
Wawili hao walifunga ndoa Juni 14, 1999, lakini waliachana mwaka 2001, huku Kim akisema Eminem alibadilika baada ya kuwa staa.
Walirudiana na kufunga ndoa nyingine mwaka 2006 lakini nayo haikudumu kwani Eminem aliomba wachache miezi minne tu baadaye.
Katika ndoa zao mbili, Eminem na Kim walibahatika kupata mtoto mmoja, binti aitwaye Hailie Jade, aliyezaliwa Desemba 25, 1995.
Hata hivyo, Eminem alikubali kumuasili binti wa Kim, Stevie Laine, ambaye bibiye huyo alimpata katika mahusiano yake na mshikaji aitwaye Eric Hartter.
Pia, wanaye binti aitwaye Alaina Marie, ambaye ni mtoto wake sasa yake Kim, Dawn. Eminem aliamua kumuasili baada ya Dawn kuingia kwenye ‘uteja’ wa dawa za kulevya na kisha kufarili mwaka 2016.
Kwa sasa, Eminem na Kim wana mjukuu aitwaye Elliot Marshall McClintock, ambaye ni mtoto wa kiume wa binti yao Hailie.
Tangu alipoachana na Kim, Eminem hajaoa na amekuwa msiri juu ya maisha yake ya mahusiano, licha ya huko nyuma kuwahi ‘kutoka’ na warembo kama Mariah Carey (2001) na Brittany Murphy (2002).


