30 C
New York

Maisha ya Diddy gerezani yanasikitisha, rufaa bado kizungumkuti

Published:

LOS ANGELES, Marekani

TIMU ya mawakili wa Sean Combs ‘Diddy’ inapambana kupinga hukumu aliyopewa rapa huyo anayeendelea kusota gerezani tangu Oktoba, 2025, akitumikia kifungo cha miezi 50 kwa makosa kadhaa, ikiwamo unyanyasaji wa kingono.

Kwamba mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 56 alikuwa akisafirisha wanawake na mabinti maeneo mbalimbali ya Marekani ili kuwauza kwa wafanyabiashara na mastaa wenzake.

Aprili, 2026, timu yake ya wanasheria iliwasilisha rufaa ya kutaka apunguziwe hukumu, wakisema Diddy hakutendewa haki kuhukumiwa miezi 50 gerezani.

Ikiwa ni miezi takribani miwili tangu rufaa hiyo iwasilishwe mahakamani, hakuna uamuzi uliochukuliwa na Diddy, ambaye ni baba wa watoto saba, amebaki kwenye kuta za gereza.

Bosi huyo wa lebo maarufu ya muziki ya Bad Boy Records, anaishi kwenye Gereza la Fort Dix, ambapo analazimika kuchangia bafu na wafungwa wengine, tofauti na alivyokuwa akiishi kwenye mjengo wake wa Dola milioni 48 mjini Miami au ule wa Dola milioni 62 ulioko Los Angeles.

Mmoja ya waliowahi kufungwa kwenye Gereza hilo na kuishi humo kwa miezi 17 kuanzia mwaka 2019 hadi 2020, anasema hali ya maisha ni mbaya kwa wafungwa.

“Kila ghorofa ina bafu moja. Vyoo na mabomba ya mvua vimeharibika. Vyakula vingi (wanavyopewa wafungwa) vimekwisha muda wake. Hali inatisha. Hakuna anayejali,” amesema katika mahojiano yake na Jarida la US.

Kwa upande wake, Diddy, licha ya ustaa wake, ikiwamo kutwaa tuzo ya Grammy, amekuwa akiishi kwa upendo na wafungwa wengine, ikiwamo kuzungumza nao na kuwapa ushauri, kwa mujibu wa mwanasheria wake, Engelmayer.

Katika baadhi ya majukumu yake gerezani, Diddy aliyekuwa na utajiri wa Dola milioni 400 mwaka 2023, amekuwa akifanya kazi maktaba, ikiwa ni pamoja na kupanga vitabu na kuziweka sawa nyaraka mbalimbali.

Pia, hukumu yake inamtaka kuhudhuria masomo juu ya matumizi ya dawa za kulevya katika Gereza la Dix. Alipokamatwa, aina tatu tofauti ya dawa za kulevya zilikutwa kwenye chumba cha hoteli aliyokuwa mjini New York.

Kwa mujibu wa mwanasheria wake, familia yake, akiwamo mama (Janice), imekuwa ikiwasiliana naye mara kwa mara kwa kumtembelea gerezani.

Awali, Diddy alitarajiwa kuachiwa Juni 4, 2028, lakini sasa huenda akarejea uraiani Aprili 25, 2028.

Related articles

Recent articles