25.4 C
New York

Maeneo 9 ya kujivunia Wizara ya Maliasili na Utalii

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jumatatu, Mei 18, 2026 limepitisha Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka Mpya wa Fedha 2026-27 Bungeni mjini Dodoma iliyowasilishwa Ijumaa Mei 15, 2026 na Waziri wa wizara hiyo, Dk. Ashatu Kijaji, Mei 15, 2026, amewasilisha

Katika hotuba yake, Dk. Kijaji amegusa maeneo mengi, lakini kubwa ni mafanikio ya kujivunia si tu kwa Wizara hiyo, bali hata nchi kwa ujumla.

ONGEZEKO LA IDADI YA WATALII

Dk. Kijaji amesema Tanzania imefanikiwa kuongeza idadi ya watalii na kufikia 5,935,561 mwaka 2025 ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.7, ikilinganishwa na watalii 5,360,247 mwaka 2024.

Aidha, amesema ongezeko hili linajumuisha watalii wa kimataifa walioongezeka kwa asilimia 7.1 kutoka 2,141,895 mwaka 2024 hadi 2,294,495 mwaka 2025 na watalii wa ndani walioongezeka kwa asilimia 13.1 kutoka 3,218,352 mwaka 2024 hadi 3,641,066 mwaka 2025.

“Ukuaji huu pia umeonekana katika mizania ya dunia, ambapo taarifa ya Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) imeonesha, kidunia Tanzania imeshika nafasi ya 11 mwaka 2025 kwa ongezeko la wageni wa kimataifa (51%), ukilinganisha na mwaka 2019 kabla ya janga la UVIKO 19.

Vilevile, Dk. Kijaji ameongeza kuwa Tanzania imekuwa ya sita kwa kanda ya Afrika, na Mashariki ya Kati kwa ongezeko la wageni wa kimataifa, ukilinganisha na mwaka 2019.

“Taarifa hizi zinaonesha uwekezaji uliofanywa na serikali ya awamu ya sita (6) unaendelea kuleta matunda mema. Pamoja na ongezeko la wageni wa kimataifa, Tanzania katika mizania ya utalii mwaka 2025 imeshika nafasi ya tatu duniani kwa soko la utalii lililofanya vizuri, ukilinganisha na 2024 ambapo watalii walitumia fedha kwa wingi (best performing market by spending).

MAPATO YA UTALII YAMEPAA ZAIDI

Aidha, Dk. Kijaji amesema kufikia Desemba 2025, mapato ya jumla yatokanayo na shughuli za utalii nchini yamepanda kutoka Dola za Marekani bilioni 3.9 mwaka 2024 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 4.4 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 12.82.

Ameeleza kuwa hatua kubwa hiyo imeifanya sekta ya utalii nchini kuwa namba mbili kwa kuingiza fedha za kigeni nchini, ikitanguliwa na sekta ya madini.

Pia, ametaja juhudi mbalimbali, ikiwemo kuongezeka kwa utangazaji utalii, uboreshaji wa miundombinu ya utalii na huduma na matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato.

USHINDI WA TUZO ZA KIMATAIFA

Kutokana na maendeo yake kwenye shughuli za utalii, Tanzania imefanikiwa kushinda tuzo mbalimbali za kimataifa, ikiwamo ya World Travel Awards.

Vilevile, Tanzania ilitangazwa kuwa Nchi Bora ya Utalii wa Safari Duniani (World’s Leading Safari Destination) mwaka 2025, ikiwa ni kwa mara ya tatu mfululizo kuanzia mwaka 2023.

Pia, Hifadhi ya Taifa Serengeti ilishinda Tuzo ya Hifadhi Bora Duniani (World’s Leading National Park 2025), ushindi unaoifanya kuendelea kuwa moja ya Maajabu ya Dunia yenye mandhari, wanyamapori na tukio la kipekee la Uhamaji wa Nyumbu (The Great Wildebeest Migration).

Sambamba na hilo, Zanzibar ilitangazwa kuwa Eneo Bora la Mikutano na Matukio ya Biashara. “Mafanikio haya yameimarisha hadhi ya Tanzania kimataifa, kuongeza ushindani wa Sekta ya Utalii katika utoaji wa huduma bora pamoja na kuchangia ongezeko la watalii na uwekezaji nchini,” amesema Dk. Kijaji.

MIUNDOMBINU YA UTALII

Kwa upande mwingine, Serikali imeendeleza uwekezaji mkubwa katika maendeleo ya miundombinu ya utalii nchini, ikiwamo kukamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege vitatu katika Hifadhi za Taifa za Nyerere (1) na Ruaha (2).

“Aidha, ujenzi wa Kiwanja cha Mikumi utakamilika kufikia Oktoba, 2026. Vilevile, Wizara imekarabati viwanja vya ndege nane katika Hifadhi za Taifa za Mikumi (1), Ruaha (2), Nyerere (2) na Serengeti (3).

“Aidha, jumla ya kilomita 3,757.92 za barabara na kilomita 523.14 za njia za watembea kwa miguu zimejengwa na kukarabatiwa katika maeneo yaliyohifadhiwa ili kurahisisha ufikaji kwenye vivutio vya utalii,” amesema Dk. Kijaji.

Wakati huo huo, miundombinu ya huduma za utalii imeimarishwa kupitia ujenzi wa maeneo sita ya mapumziko kwa wageni na malango tisa ya kuingilia wageni katika Hifadhi za Taifa za Nyerere, Mikumi na Ruaha, pamoja na vituo vya utalii katika misitu ya Meru, Vikindu, Mwambesi, Pindiro, Mlima Rungwe na Ziwa Duluti.

Sambamba na hilo, kambi moja (1) ya watalii imejengwa katika Hifadhi ya Misitu ya Mazingira Asilia ya Kilombero. “Uwekezaji huu umeleta matokeo chanya yanayoonekana kwa kuongeza urahisi wa kufikia vivutio vya utalii, kuboresha uzoefu wa wageni na kufungua fursa za ajira na biashara kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi,” amesema.

SENSA YA WANYAMAPORI

Katika hotuba yake, pia Dk. Kijaji ameeleza namna Wizara ya Maliasili na Utalii inavyojivunia kukamilisha zoezi la sensa ya kitaifa ya wanyamapori nchini.

“Sensa kama hii ni ya pili kufanyika na hufanyika kila baada ya miaka 10, ikiwa ni sehemu ya Mpango wa Kitaifa wenye lengo la kubaini uwepo, idadi, mtawanyiko na mienendo ya wanyamapori, sambamba na kubaini viashiria hatarishi vinavyoweza kuathiri ustawi na mazingira yao kwa kulinganisha na matokeo ya awali,” amesema.

Kubwa zaidi kwa Wizara, Sensa hiyo imefanyika kwa kutumia fedha za ndani kwa mara ya kwanza, tofauti na sensa ya awali, hatua inayodhihirisha uwezo na dhamira ya Serikali katika kugharamia na kusimamia shughuli za kimkakati za uhifadhi.

“Matokeo ya sensa yanaonesha mwenendo chanya wa ongezeko na ustawi wa wanyamapori katika mifumo ikolojia mbalimbali, hali inayothibitisha mafanikio ya juhudi za Serikali katika kuimarisha uhifadhi endelevu wa rasilimali hizi.

“Aidha, takwimu zilizopatikana ni nyenzo muhimu katika kupanga matumizi bora ya rasilimali ikiwemo uwindaji endelevu, kubaini na kulinda jamii za wanyamapori zilizo hatarini kutoweka pamoja na kusaidia kupanga mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto za shughuli za kibinadamu katika mifumo ikolojia,” amesema Dk. Kijaji.

SOKO LA ASALI KIMATAIFA

Dk. Kijaji ameongeza pia, kwamba kiwango cha asali ya Tanzania kinachouzwa nje ya nchi kimeongezeka kutoka tani 951.6 mwaka 2024 hadi tani 1,596.8 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 67.85.

“Aidha, thamani ya mauzo ya asali imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 11.4 kwa mwaka 2024 hadi Shilingi bilioni 19.2 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 68.4,” amesema.

Kufanikisha mafanikio hayo, amezitaja jitihada za Serikali katika kuimarisha Sekta ya Ufugaji Nyuki na upatikanaji wa masoko ya kimataifa, pia wafugaji nyuki na wadau wa maendeleo kwa kuongeza kiwango cha uzalishaji wa asali inayokidhi viwango vya kimataifa.

Pia, amesema asali ya Tanzania imeendelea kukidhi ubora kwa wastani wa asilimia 97 kwa viwango vya Umoja wa Ulaya kwa miaka mitatu mfululizo, jambo lililoongeza fursa za masoko ya nje katika nchi za Marekani, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Falme za Kiarabu, na China.

Aidha, Dk. Kijaji ameeleza kuwa kwa mara ya kwanza, asali ya Tanzania imefanikiwa kuuzwa katika soko la Uingereza baada ya kukidhi vigezo.

TANZANIA NA URITHI WA DUNIA

Taswira ya Tanzania katika sekta ya utalii imeendelea kung’arishwa na umahiri wake katika uhifadhi na usimamizi wa maeneo ya urithi wa Dunia, ambapo imechaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia katika kipindi cha miaka minne (4) kuanzia mwaka 2025 hadi 2029.

Akifafanua zaidi, Dk. Kijaji amesema: “Kwa nafasi hiyo, Tanzania imeingia katika chombo cha juu cha UNESCO chenye jukumu la kufanya maamuzi kuhusu uhifadhi na usimamizi wa maeneo ya urithi wa Dunia kinachojumuisha nchi 21 kati ya 195.

“Kupitia ujumbe huo, Tanzania ina fursa ya kushiriki katika maamuzi ya kuongeza au kuondoa maeneo katika orodha ya urithi wa Dunia.”

UJENZI, UZINDUZI WA JIOPAKI YA NGORONGORO-LENGAI

Katika hotuba yake, Dk. Kijaji amesema Wizara imekamilisha ujenzi wa miundombinu ya utalii na kuzindua Makumbusho ya kisasa ya Jiopaki ya Ngorongoro-Lengai iliyopo katika eneo la Kamyn Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, ambayo ni makumbusho ya pili ya aina hiyo barani Afrika baada M’Guon iliyopo Morocco.

“Hatua hii imeongeza zao jipya la utalii wa jiolojia ambalo pia litakuza utafiti wa kisayansi na elimu ya miamba, kuwezesha jamii na wanafunzi kujifunza historia ya sayansi na mazingira, kuongeza ajira na kipato kwa wananchi wa maeneo jirani na kuimarisha nafasi ya Tanzania kimataifa kama kinara wa uhifadhi, utalii na elimu ya miamba,” amesema.

Aidha, ameongeza kuwa hatua hiyo ni miongoni mwa mikakati ya Wizara katika kuliongezea thamani Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ambalo mwaka 2018 lilipewa hadhi ya jiopaki inayotambuliwa na UNESCO na kuwa jiopaki pekee yenye hadhi hiyo katika Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

MAGEUZI YA KIDIGITALI

Dk. Kijaji ameeleza pia namna Wizara ya Maliasili na Utalii ilivyofanikisha maboresho ya mfumo wa MNRT Portal, ambao umekuwa ukitumiwa na Wizara pamoja na taasisi katika kusimamia utoaji wa huduma mbalimbali, ikiwemo leseni za shughuli za utalii, huduma za malazi, uwindaji wa kitalii, minada ya vitalu na vibali vya kuingia katika vivutio vya utalii.

Amesema: “Maboresho hayo yamelenga kuboresha uzoefu wa watumiaji, kuhuisha teknolojia ili mfumo uweze kuendana na mahitaji ya sasa pamoja na kufungamanisha na mifumo mingine inayotoa huduma za utalii na kurahisisha utoaji wa huduma kufanyika kwa ufanisi na tija.

“Wizara imeanzisha mfumo wa ‘Problem Animals Information System (PAIS)’, mahsusi kwa ajili ya kusimamia taarifa za matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na kuratibu na kuwezesha ulipaji wa vifuta jasho/machozi kwa wananchi wanaoathirika na matukio hayo.”

Akizungumzia faida za mabadiliko hao, Dk. Kijaji amesema Mfumo huo umerahisisha ukusanyaji, uwasilishwaji wa taarifa sahihi na kuepuka udanganyifu, uchakataji, utunzaji wa taarifa za matukio ya uharibifu wa wanyamapori wakali na waharibifu.

“Vilevile, mfumo umerahisisha malipo ya kifuta jasho na machozi kwa wananchi waliopata madhara ya wanyamapori wakali na waharibifu ambapo kwa sasa taratibu za malipo zinachukua siku saba hadi 14, tofauti na taratibu za awali ambapo malipo yakichukua miezi sita hadi 12.

“Sambamba na hilo, mfumo umeongeza uwazi na uwajibikaji kwa kuwa mfumo unawezesha kufuatilia kila muamala. Kufuatia agizo la kufungamanisha mifumo ya Serikali lililotolewa na Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara imeanzisha jukwaa la kidijitali (FARU GATEWAY) la kubadilishana taarifa kati ya mifumo ya Wizara na Taasisi zake.”

Dk. Kijaji amesema Jukwaa hilo limefungamanishwa na Mfumo wa Serikali wa Kuwasiliana na Kubadilishana Taarifa (GovESB), hivyo kufanya taarifa za Sekta ya Maliasili na Utalii kubadilishana taarifa na Taasisi zilizopo katika sekta nyingine za Serikali, hatua hii imeongeza ufanisi, tija na ushirikiano katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kama hiyo haitoshi, Wizara imeendelea kufanya mageuzi ya kidijitali katika Sekta ya Utalii kwa kuanzisha mfumo wa kisasa unaojulikana kama Tanzania Travel Companion, ambao ni sehemu ya utekelezaji wa kituo cha Uendeshaji wa Masoko ya Utalii Kidijitali (DDMCC).

Amesema: “Mfumo huo umelenga kuboresha uzoefu wa mtalii (travel experience) kuanzia hatua ya upangaji wa safari, wakati wa safari na baada ya safari. Aidha, kupitia mfumo huo watalii wataweza kupanga safari zao kabla ya kuwasili nchini kwa kupata taarifa sahihi, kufanya ‘booking’ ya huduma mbalimbali zikiwemo malazi, migahawa, usafiri na vivutio vya utalii, pamoja na taarifa kuhusu maeneo ya vivutio yasiyo maarufu (hidden gems) yaliyopo katika miji yetu.

“Vilevile, mfumo umefungamanishwa na Mifumo ya Taasisi za Wizara ili kurahisisha malipo ya huduma mbalimbali ikiwemo ada za viingilio, malazi katika hoteli/loji, kambi za kitalii na magari katika vivutio kwa lengo la kuongeza ufanisi na kupunguza gharama katika ukusanyaji wa mapato.”

Ifahamike kuwa Mfumo huo pia umejumuisha ramani ya kidijitali ya vivutio na huduma muhimu kwa watalii pamoja na ‘chatbot’ ya akili-unde (AI Chatbot) itakayotoa mwongozo wa papo kwa papo kwa watalii kwa lugha za kimataifa zaidi ya 56.

Kwa upande mwingine, ni Mfumo unaotarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika maandalizi na wakati wa michuano ya AFCON 2027 kwa kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na huduma za utalii kwa urahisi kwa wageni watakaotembelea nchi yetu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img