NEW YORK, Marekani
NI kwa mujibu wa Mpango wa Ukimwi wa Umoja wa Mataifa (UNAIDS), ikielezwa kuwa vita dhidi ya Ukimwi imepungua duniani kutokana na kushuka kwa uwekezaji wa fedha.
UNAIDS imeeleza kuwa mifumo ya huduma za afya imedorora katika mataifa mengi duniani, hivyo kuathiri mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima, amesema dunia imerudi nyuma, badala ya kusonga mbele katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Byanyima amesema hayo katika mazungumzo yake na waandishi wa habari yaliyofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York, Marekani.
“Leo hii, watu milioni 9.3 wanaoishi na virusi vya Ukimwi bado hawajaanza matibabu na maambukizi yalifikia milioni 1.3 kwa mwaka 2024,” amesema Byanyima.
Aidha, Byanyima ameeleza kuwa mifumo ya afya katika nchi nyingi imedorora kutokana na wahisani, ikiwamo Marekani, kusitisha misaada kwenye eneo hilo la mapambano dhidi ya Ukimwi.
Katika nchi zote nane ambako UNAIDS inafanya kazi, zinategemea kwa asilimia 99.9 michango ya wahisani wa nje katika kukabiliana na Ukimwi.
Hivyo, kitendo cha wahisani kukaa kando au kupunguza misaada, kimeathiri kwa kiasi kikubwa programu za kuzuia maambukizi au kutoa tiba.
Licha ya takwimu za mwaka 2024 kuonesha kuwa mabinti na wanawake takribani 570 hupata maambukizi ya Ukimwi kila siku, asilimia 60 ya taasisi zinazosaidia makundi hayo zimesitishiwa misaada barani Afrika.
Athari zake zimeonekana nchini Uganda, ambako utoaji wa dawa za PrEP (pre-exposure prophylaxis) zinazozuia maambukizi kwa asilimia hadi 99 ulishuka kwa asilimia 31 kuanzia Desemba 2024 hadi Septemba, 2025.

Kama hiyo haitoshi, asilimia 45 ya programu za Ukimwi zimesitishwa. Ni kama ilivyo kwa Burundi, ambako utoaji wa kinga hiyo uliporomoka kwa asilimia 64 katika kipindi kama hicho.
Aidha, kwa mujibu wa UNAIDS, utoaji wa zana kama kondomu nao umeshuhudiwa ukipitia changamoto kubwa.
Hilo limeonekana wazi nchini Nigeria, ambako utoaji wa zana hizo za kujikinga na Ukimwi ulishuka kwa asilimia 55 kuanzia Desemba 2024 hadi Machi, 2025.
Kenya, kwa upande wake, asilimia kubwa ya vituo vilivyokuwa vikihudumia waathirika wa Ukimwi wa makundi maalumu, vimefungwa. Ni kama ilivyo kwa Nigeria.
Zimbabwe, ambako ‘madada poa’ walikuwa wakipimwa, kupewa kinga na matibabu, huduma hizo zimeporomoka kwa kiwango kikubwa tangu mwaka 2025.


