16.1 C
New York

Tanzania yaandika historia soko la helium

Published:

Na Mwandishi wetu, Gazetini

TANZANIA imeanza rasmi safari mpya ya kihistoria katika sekta ya madini baada ya kuingia kwenye ramani ya dunia kama mzalishaji na msambazaji wa kimkakati wa gesi ya helium, kufuatia kusainiwa kwa Mkataba wa Uchimbaji wa Gesi hiyo kati ya Serikali na kampuni ya Helium One Global Limited kupitia Kampuni ya Ubia ya Songwe Helium Limited. Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika Mei 2, 2026 mkoani Songwe, hatua inayofungua ukurasa mpya wa uwekezaji katika rasilimali adimu yenye matumizi makubwa duniani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, amesema Tanzania sasa inaingia katika kundi la mataifa yatakayokuwa na mchango wa moja kwa moja kwenye usambazaji wa helium duniani,

soko ambalo kwa sasa linatawaliwa na nchi chache tu zikiwemo Marekani na Qatar zinazochangia zaidi ya asilimia 75 ya uzalishaji wote wa gesi hiyo. Amesema pamoja na nchi kama Urusi, Algeria, Canada, China na Poland kushiriki katika uzalishaji, bado dunia inakabiliwa na uhaba wa helium kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji ya kimataifa.

Kwa mujibu wa Dk. Kiruswa, mahitaji ya helium duniani tayari yamevuka futi za ujazo bilioni 6 kwa mwaka na yanatarajiwa kuongezeka hadi zaidi ya futi za ujazo bilioni 8.5 ifikapo mwaka 2030, hali inayoifanya Tanzania kuingia katika soko lenye thamani kubwa na ushindani mdogo. Amesema mradi wa Southern Rukwa unaipa Tanzania nafasi ya kuwa mdau muhimu katika soko hilo na hata kuathiri mwenendo wa bei na upatikanaji wa helium duniani.

Huu ni utekelezaji halisi wa falsafa ya Serikali ya Dk. Samia Suluhu Hassan kwamba rasilimali za nchi lazima ziwe chanzo cha ustawi wa taifa,” amesema Dk. Kiruswa.

Katika mkataba huo, Serikali ya Tanzania itamiliki asilimia 17 ya hisa katika kampuni ya ubia ya Songwe Helium Limited kupitia mfumo wa hisa huru zisizohafifishwa thamani, hatua itakayowezesha taifa kushiriki moja kwa moja katika maamuzi ya kimkakati ya mradi huo na kunufaika kupitia gawio, mrabaha, kodi na tozo mbalimbali.

Dk. Kiruswa amesema mbali na mapato ya moja kwa moja kwa Serikali, mradi huo utachochea ajira kwa vijana, kuimarisha biashara za wazawa kupitia huduma za ugavi, kuboresha miundombinu ya barabara na huduma za jamii katika maeneo ya mradi, pamoja na kuongeza fedha za kigeni nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Helium One Global Limited, Lorna Blaisse, amesema utiaji saini wa mkataba huo ni hatua muhimu si kwa Tanzania pekee bali pia kwa soko la helium duniani, akieleza kuwa mradi huo una akiba yenye uwezo mkubwa wa uzalishaji wa kibiashara. Amesema mafanikio ya awali ya uchimbaji katika kisima cha Itambula West-1 mwaka 2024 yalithibitisha uwepo wa helium kwa kiwango kikubwa.

Katika upimaji wa kisima uliopanuliwa robo ya tatu ya 2024, kisima cha ITW-1 kilirekodi helium yenye mkusanyiko wa asilimia 5.5 hadi juu ya ardhi, na hadi asilimia 7.6 kutoka miamba ya Karoo iliyovunjika na miamba ya Basement iliyopasuka,” amesema Blaisse.

Ameongeza kuwa baada ya kusainiwa kwa leseni ya uchimbaji, kampuni ya Songwe Helium Limited sasa itaendelea na hatua za mwisho za maandalizi kuelekea uzalishaji wa kwanza wa kibiashara wa helium nchini. Hatua hizo ni pamoja na kukamilisha mipango ya maendeleo ya mradi, tathmini ya athari za mazingira na jamii, usanifu wa miundombinu pamoja na ununuzi wa vifaa vya uchakataji na usafirishaji wa helium.

Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano ya Wizara ya Madini, Profesa Sifuni Mchome, amesema mfumo wa Serikali kumiliki hisa katika miradi ya madini unaendelea kuzaa matunda kwa kuhakikisha taifa linanufaika moja kwa moja na rasilimali zake huku likiwa sehemu ya maamuzi ya msingi ya miradi mikubwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Makame, amesema mkoa huo unaendelea kujipambanua kama kitovu kipya cha uwekezaji wa madini kutokana na uwepo wa rasilimali mbalimbali zikiwemo helium na rare earth elements, huku akiahidi ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.

Helium ni miongoni mwa gesi adimu zaidi duniani na haina mbadala wa moja kwa moja katika matumizi yake ya kisasa. Hutumika katika vifaa vya tiba kama MRI, utengenezaji wa vifaa vya kielektroniki na teknolojia za kidijitali, sekta ya anga, ulinzi, tafiti za kisayansi, fibre optics na hata teknolojia za kisasa kama quantum computing.

Kwa kuanza kwa mradi huo wa kihistoria, Tanzania sasa inajiweka kwenye nafasi mpya ya kimkakati katika uchumi wa madini duniani, huku ikitarajiwa kunufaika si tu kwa mapato, bali pia kwa hadhi ya kuwa miongoni mwa mataifa machache yenye uwezo wa kuzalisha na kusambaza gesi hiyo muhimu duniani.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img