9.5 C
New York

Changamoto zinazomsubiri bosi mpya wa Apple

Published:

NEW YORK, Marekani

KAMPUNI kubwa ya teknolojia dunini ya Apple Inc. imetangaza kuwa mtendaji wake wa muda mrefu, John Ternus, atachukua nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji (CEO) kuanzia Septemba 1, akirithi nafasi hiyo kutoka kwa Tim Cook.

Katika taarifa iliyotolewa rasmi, Ternus amesema amebahatika kufanya kazi kwa muda mrefu ndani ya Apple, akijifunza chini ya mwanzilishi wake Steve Jobs pamoja na kupata malezi ya kiuongozi kutoka kwa Cook.

Anafanya kazi gani Apple?

Kwa sasa, Ternus ni Makamu wa Rais Mwandamizi wa Uhandisi wa Vifaa (Senior Vice President of Hardware Engineering) ndani ya Apple. Katika nafasi hiyo, ameongoza maendeleo ya bidhaa kuu za kampuni hiyo, zikiwemo iPhone na Mac, pamoja na ubunifu mpya kama Apple Vision Pro.

Amehusika kwa karibu katika ukuzaji wa bidhaa mpya kama MacBook Neo na mfululizo wa iPhone 17, huku timu yake ikitajwa kuwa kiini cha mafanikio ya bidhaa hizo.

Muda wake ndani ya Apple

Ternus ana zaidi ya miaka 25 ndani ya Apple. Alijiunga na kampuni hiyo mwaka 2001 katika kitengo cha ubunifu wa bidhaa, kabla ya kupanda ngazi na kuwa Makamu wa Rais wa Uhandisi wa Vifaa mwaka 2013. Mwaka 2021, aliteuliwa kuwa sehemu ya timu ya juu ya uongozi wa kampuni.

Kabla ya kujiunga na Apple, alifanya kazi kama mhandisi katika kampuni ya Virtual Research Systems, na ana shahada ya uhandisi wa mitambo kutoka Chuo Kikuu cha Pennsylvania.

Kwa mujibu wa wachambuzi, kupandishwa kwake hakujaja kama mshangao, kwani alikuwa akitajwa kwa muda kama mmoja wa wanaotarajiwa kurithi nafasi ya CEO.

Ternus anachukua nafasi hiyo katika kipindi ambacho Apple imefikia thamani ya soko ya dola trilioni 4 chini ya uongozi wa Tim Cook. Hata hivyo, changamoto kubwa inayomkabili ni mwelekeo wa kampuni katika teknolojia ya akili bandia (AI).

Wachambuzi wanasema kuna matarajio makubwa kwake kuhakikisha Apple inaendelea kuwa kinara wa ubunifu, hasa katika ushindani mkali wa teknolojia za AI duniani.

Tofauti na Steve Jobs aliyekuwa maarufu kwa ubunifu wa hatari, na Cook aliyefanikiwa kupitia huduma na maboresho ya bidhaa zilizopo kama Apple Watch, AirPods na Apple TV+, sasa macho yote yanaelekezwa kwa Ternus kuona ataelekea njia ipi.

Kwa kuwa ni mtaalamu wa vifaa (hardware engineer), baadhi ya wachambuzi wanaamini ataweka mkazo katika ubunifu wa vifaa vinavyoweza kutoa uzoefu mpya wa kidijitali, huku Apple ikijipanga kujiimarisha zaidi katika enzi ya AI.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img