24.5 C
New York

PBPA yatoa elimu kuhusu mfumo wa uagizaji mafuta kwa pamoja

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

WAKALA wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) unasimamia Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja, ambao umeisaidia Serikali kuhakikisha bidhaa za mafuta ya petroli, zinapatikana nchini kwa uhakika, kwa wakati na kwa gharama shindani.

Mwanasheria wa PBPA, Khadija Zuberi, amesema hayo wakati akitoa elimu kwa wananchi katika Maonesho ya Nanenane jijini Dodoma kuhusu namna mfumo huo unavyofanya kazi na fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya mafuta.

Amesema mfumo huo unahusisha makundi mawili muhimu ambayo ni Kampuni za Uuzaji wa Mafuta (OMCs) zilizosajiliwa nchini na kupewa leseni na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), pamoja na kampuni zilizohakikiwa na kuidhinishwa kushiriki katika zabuni za kuingiza mafuta nchini.

“Katika mfumo wetu tuna kampuni za mafuta zilizosajiliwa nchini na kupewa leseni na EWURA. Pia tuna kampuni zilizohakikiwa na kuidhinishwa kushiriki katika zabuni za kuingiza mafuta nchini,” amesema Zuberi.

Ameeleza kuwa kampuni inayotaka kusajiliwa na PBPA, pamoja na mambo mengine, inapaswa kuwa na leseni halali kutoka EWURA, nyaraka za usajili wa biashara kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), pamoja na kutimiza masharti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kwa mujibu wa Bi. Zuberi, baada ya kampuni kukamilisha usajili, inatakiwa kuwasilisha kwa taasisi mahitaji yake ya mafuta kila mwezi. Mahitaji ya kampuni zote hukusanywa na kutumika kuandaa zabuni ya kupata kampuni itakayoingiza mafuta nchini.

“Tunapopokea mahitaji ya kila mwezi kutoka kwa kampuni za mafuta, tunayakusanya na kuendesha mchakato wa zabuni kwa uwazi na ushindani. Kampuni inayokidhi masharti na kutoa bei shindani huchaguliwa kuingiza mafuta nchini,” amesema.

Amesema kuunganisha mahitaji ya kampuni mbalimbali na kuagiza mafuta kwa pamoja kunaiwezesha nchi kutumia faida ya ununuzi wa kiasi kikubwa, kupata bei shindani za usafirishaji na kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa mafuta.

Zuberi amewahimiza Watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta ya mafuta kwa kuanzisha kampuni na shughuli nyingine zinazohusiana na biashara hiyo, huku wakizingatia masharti ya kisheria na kitaalamu.

Related articles

Recent articles