24.5 C
New York

Chadema yakana kufanya mazugumzo na Serikali

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KATIBu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema, John Mnyika, amesema chama hicho pamoja na Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, hadi sasa hawajafanya mazungumzo yoyote na Serikali, akipinga kauli iliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu uwepo wa mazungumzo na kiongozi wa chama cha siasa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Agosti 3, 2026, Mnyika alisema kauli ya Rais Samia iliyotolewa Julai 30, 2026, wakati wa mkutano na viongozi wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, haikuhusu Chadema wala Mwenyekiti wake.

Kwa mujibu wa Mnyika, uongozi wa Chadema ulimtafuta Tundu Lissu ili kupata ufafanuzi kuhusu suala hilo, ambapo Lissu alieleza kuwa tangu mazungumzo yake na Rais Mstaafu wa Malawi, Lazarus Chakwera, hajafanya mazungumzo yoyote na Serikali au mtu mwingine yeyote kuhusu mchakato huo.

Mnyika alisema kutokana na hali hiyo, Chadema inaendelea kushikilia msimamo wake na kuwataka viongozi pamoja na wanachama wa chama hicho kuendelea kuwa na umoja na kusubiri maelekezo rasmi ya uongozi.

Julai 30, 2026, Rais Samia Suluhu Hassan alikutana na viongozi wa vyama 18 vya siasa vyenye usajili wa kudumu, huku CHADEMA ikiwa chama pekee ambacho hakikushiriki mkutano huo. Akizungumza katika mkutano huo, Rais alisema:

“Mwenzetu mmoja bado anaendelea kutafakari, bado tunaendelea kupokea misukumo yake, conditions zake, matakwa yake ndiyo.”

Kauli hiyo ndiyo ambayo Mnyika amesema haikuhusu Chadema, akisisitiza kuwa hadi sasa hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika kati ya chama hicho na Serikali.

Related articles

Recent articles