NEW YORK, Marekani
Bilionea maarufu duniani, Elon Musk, ameweka historia mpya baada ya kuwa mtu wa kwanza kumiliki utajiri unaozidi dola bilioni 800, kufuatia hatua ya kampuni yake ya kutengeneza roketi, SpaceX, kununua kampuni ya akili mnemba (AI) ya xAI.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Forbes, ununuzi wa xAI uliothaminiwa kufikia dola trilioni 1.25 umeongeza utajiri wa Musk kwa dola bilioni 84, na kuufikisha utajiri wake jumla ya dola bilioni 852.
Kabla ya muamala huo, Musk alikuwa anamiliki asilimia 42 ya SpaceX, kampuni iliyokuwa na thamani ya dola bilioni 336, huku mwezi Desemba mwaka jana ikikadiriwa kufikia thamani ya dola bilioni 800.
Aidha, Musk alikuwa anamiliki asilimia 49 ya kampuni ya xAI, ambayo awali ilikuwa na thamani ya dola bilioni 122, kabla ya kampuni hiyo kupandishwa thamani hadi dola bilioni 250. Baada ya ununuzi huo, Forbes inaeleza kuwa Musk sasa anamiliki asilimia 43 ya kampuni hiyo kwa ujumla, yenye thamani ya dola bilioni 542.
Hatua hiyo imemfanya Musk kuendelea kushikilia nafasi ya mtu tajiri zaidi duniani.
Mbali na SpaceX na xAI, tajiri huyo pia anamiliki asilimia 12 ya kampuni ya kutengeneza magari ya umeme ya Tesla, ambayo thamani yake inakadiriwa kufikia dola bilioni 178, huku hisa zake binafsi katika kampuni hiyo zikithaminiwa kuwa dola bilioni 124.
Kando na hilo, Musk alipokea malipo makubwa ya fidia (malipo ya bodi ya wakurugenzi) kutoka Tesla mwezi Novemba, yaliyokadiriwa kufikia dola trilioni 1 kabla ya kukatwa kodi.
Ikumbukwe kuwa mwezi Machi mwaka uliopita, Musk alitangaza kuunganishwa kwa kampuni ya xAI na mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), katika makubaliano ya kibiashara yaliyothamini xAI kwa dola bilioni 80 na X kwa dola bilioni 33.
Hata hivyo, hatua za Musk kuwa mnunuzi na muuzaji wa kampuni anazozimiliki mwenyewe zimeibua maswali kutoka kwa wachambuzi wa masoko, hasa kuhusu uhalisia wa ukadiriaji wa thamani ya kampuni hizo na athari zake kwa uwazi wa biashara zake.


