11.2 C
New York

Visual| Usajili wa watangazaji mapinduzi na hamahama kwenye redio Bongo

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KWA miaka ya hivi karibuni, wamiliki wa vituo vya redio na runinga hapa nchini wameshuhudiwa wakitunishia msuli wa fedha kwa kunyang’anganya baadhi ya watangazaji wenye majina makubwa.

Kama itakumbukwa, hivi karibuni bosi wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga, amekitikisa kituo cha redio cha EFM kwa kumchukua mtangazaji wa kiwango cha juu, Veronica Frank ‘Veronica Simulizi’.

Hakuishia hapo. Kusaga ‘alichana pochi’ kwenda kituo cha East Afrika Radio kumchukua aliyekuwa staa wa kipindi cha ‘Dadaz’, Najma Paul.

Hata hivyo, Veronica Simulizi na Najma ni mwendelezo tu wa mtindo mpya wa mabosi wa vituo vya redio na runinga kuzidiana kete kwa kupokonyana watangazaji maarufu.

Gardner G Habash

Ilikuwa ni Oktoba 31, 2014, ambapo EFM ya bosi Francis Ciza ‘Majizo’ iliitikisa tasnia ya utangazaji wa vipindi vya redio kwa kumchukua Gardner kutoka aliyekuwa Clouds, ambako akisifika kwa uwezo wake wa kuendesha kipindi cha jioni cha ‘Jahazi’.

Baada ya miaka miwili ya kufanya kazi EFM, Gardner (sasa marehemu) aliendeleza ubora wake kupitia kipindi cha ‘Ubaoni’, kabla ya kurudi Clouds mwaka 2016.

Paul James ‘PJ’ & Gerald Hando

Aprili 9, 2016, kituo cha redio cha EFM kiliwatambulisha watangazaji hao kuwa sehemu ya timu yao ya vipindi. PJ na Hando walinyakuliwa kutoka Clouds.

Hata hivyo, Oktoba 5, mwaka huo, PJ alirudi Clouds. Hatua hiyo ilisababisha mgogoro mkubwa kati yake na uongozi wa EFM uliodai amevunja mkataba kinyemela.

Maulid Kitenge

Oktoba 17, 2019, akitokea EFM Radio iliyomng’oa Radio One, Kitenge alijiunga na Wasafi FM inayotajwa kumilikiwa na supastaa wa Bongo Fleva, Nassib Abdul ‘Diamond’.

Hata hivyo, baada ya miaka miwili ya kuhudumu akiwa Wasafi, Kitenge alirejea nyumbani (EFM) na kutambulishwa rasmi Agosti 6, 2021.

Ilipofika Aprili 23, 2023, Wasafi ilimrejesha Kitenge na ameendelea kuwa mtumishi wa kituo hicho hadi sasa.

Zembwela

Oktoba 23, 2019 ilikuwa ni siku nzuri kwa wapenzi na wasikilizaji wa Wasafi, ambapo kituo hicho kilimtambulisha Hilary Daudi ‘Zembwela’ kuwa mtangazaji wake mpya.

Ikumbukwe, Zembwela aliajiriwa na Wasafi akitokea East Afrika Radio, ambako ndiko alikojizolea umaarufu mkubwa kwenye masikio ya wasikilizaji.

B Dozen

Juni 3, 2020 ni siku ambayo mmiliki wa EFM, Majizo, aliitikisa tasnia ya utangazaji wa vipindi vya redio na runinga nchini alipotangaza usajili wa Hamisi Mandi ‘B Dozen’.

B Dozen, maarufu pia kwa jina la ‘B Twangala’ alikukuwa nguzo imara ya kipindi cha burudani cha ‘XXL’ na alirejea nyumbani (Clouds) na kutambulishwa Juni 22, 2023.

Dulla Planet

Aprili 14, 2024, itakumbukwa kuwa Crown FM kikiwa kituo kipya cha redio, kilimtambulisha mtangazaji nyota wa vipindi vya burudani, Dulla Planet.

‘Mjukuu wa Ambua’ alihamia Crown FM ya staa wa Bongo Fleva, Ali Kiba, akitokea EATV na East Africa Radio, ambako alitengeneza jina kubwa kupitia kipindi cha ‘Planet Bongo’ alichoachiwa na Salama Jabir.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img