Na mwandishi wetu, Gazetini
PIKIPIKI ni chombo cha matairi matau kilichojizolea umaarufu mkubwa katika sekta ya usafirishaji.
Wengi wanapoziita ‘bodaboda’ hulenga pikipiki za biashara, ingawa msingi wa jina hilo ni uwezo wa vyombo hivyo kupenya katika mazingira yanayozuia magari kuingia, ikiwamo vichochoroni.
Pia, ushawishi wa pikipiki kwa watu wengi unatokana na urahisi wa vyombo hivyo kupenya na kuepuka msongamano wa magari barabarani.
Sasa, kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya World Population Review, India ndiyo nchi yenye pikipiki nyingi, zikitajwa kufikia milioni 221 zilizopo barabarani wa sasa.
Kama ilivyo duniani kote, pikipiki katika Taifa hilo la barani Asia lenye watu bilioni 1.3 hutumika kwa matumizi ya biashara na hata usafiri binafsi.
Indonesia inashika nafasi ya pili, kwa mujibu wa World Population Review, ikiwa na pikipiki milioni 112. Kwa Indonesia, ni chombo cha usafiri wa familia, ingawa pia hutumika kwa biashara.
Nafasi ya tatu katika orodha ya nchi zenye pikipiki nyingi inashikwa na China, zikitajwa kufikia milioni 85 kwa takwimu za hivi karibuni.
Taifa jingine la Asia, Vietnam, inashika nafasi ya nne ikiwa na pikipiki milioni 58, ambapo familia nyingi za kipato cha kati zimeonekana kuvutiwa na usafiri huo.
Thailand, Malaysia na Taiwan nako usafiri wa pikipiki umejizolea umaarufu wa kutosha. Kwa Thailand, kuna pikipiki milioni 22, ikifuatiwa na Malaysia (milioni 15) na Taiwani (milioni 14).
Aidha, Brazil imekuwa nchi pekee nje ya Asia kuingia ‘Top 10’ ya mataifa yenye pikipiki nyingi duniani. Taifa hilo la Amerika ya Kusini lina pikipiki milioni 10.


