Na mwandishi wetu, Gazetini
KWA mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu duniani, kwa sasa idadi ya vijana waliozaliwa kati ya mwaka 1997 na 2012 (Generation Z) ni bilioni 1.9.
Idadi hiyo ni sawa na asilimia 22.9 ya watu duniani kote, hivyo ‘Gen Z’ wanashika nafasi ya pili kwa wingi, huku Gen A wakiendelea kuongoza.
‘Gen A’ (Generation Alpha) ni kundi la watu waliozaliwa kati ya mwaka 2013 na 2024, ambao ndiyo wengi zaidi duniani wakitajwa kufikia bilioni 2, sawa na asilimia 24.4 ya watu wote.
Kundi linalofuata kwa idadi kubwa duniani ni ‘Millennials’, kwa maana ya watu waliozaliwa kati ya mwaka 1981 hadi 1996.
Kwa takwimu za Shirika hilo, watu wake ni bilioni 1.7, ambao ni sawa na asilimia 21.2 ya watu wote waliopo duniani kwa sasa.
Katika takwimu hizo, ‘Gen X’ ambao ni watu waliozaliwa kati ya mwaka 1965 hadi 1980 ni bilioni 1.4, wakati wale wa ‘Baby Boomers’ waliozaliwa kati ya mwaka 1946 hadi 1964 wakiwa ni bilioni 1.1.
Kuziweka sawa takwimu, kundi la wazee limetajwa kuwa ni asilimia 2 pekee ya watu waliopo duniani katika karne hii ya 21.


